Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WATAFITI kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameitaja mbegu ya zabibu aina ya Makutupora Nyekundu kuwa ina sifa za kipekee zinazoiweka katika daraja la juu duniani.
Akizungumza katika mahojiano na kituo kimoja cha redio jijini Dodoma leo Julai 30, 2025 Mtafiti Mwandamizi kutoka TARI Kituo cha Makutupora, Felista Mpore amesema mbegu hiyo imekuwa ya kipekee kutokana na kiwango kikubwa cha sukari kinachopatikana ndani yake.

“Mbegu ya Makutupora Nyekundu ina uwezo mkubwa wa kutoa sukari kwa kiwango cha juu, ambacho ni miongoni mwa viashiria muhimu vya ubora katika sekta ya usindikaji wa zabibu,” amesema.
Mbali na kiwango cha sukari, mbegu hiyo pia ina uwezo wa kustahimili magonjwa, kuhimili ukame, kutoa mavuno mengi, pamoja na kuwa na rangi mbalimbali zinazovutia watumiaji.
Kwa mujibu wa Mpore, watafiti kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakifika nchini kuchukua sampuli za vinasaba kwa ajili ya kulinganisha na aina nyingine za zabibu duniani, ambapo matokeo yamebainisha kuwa Makutupora Nyekundu ina sifa za kipekee zinazoiweka katika kundi la zabibu bora zaidi duniani.
Katika kuunga mkono jitihada za kuongeza thamani ya zao hilo, TARI imeendelea kutoa mafunzo kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo, ikilenga kuwajengea uwezo katika kuongeza tija kupitia usindikaji na masoko ya kisasa.
“Tunawahimiza wakulima wajikite katika kuongeza thamani ya zabibu badala ya kuuza ghafi. TARI itaendelea kutoa elimu na mafunzo, hususan kuelekea Maonesho ya Kilimo ya Nanenane ambapo tutakuwepo katika viwanja mbalimbali, ikiwemo vile vya kitaifa vilivyopo Nzuguni, Dodoma,” amesema.
Zabibu ya Makutupora Nyekundu hulimwa kwa wingi katika maeneo ya kati nchini Tanzania, hususan Mkoa wa Dodoma, na imekuwa chanzo kikuu cha malighafi kwa viwanda vya ndani vya utengenezaji wa mvinyo.