Na Lucy Ngowi
MOROGORO: SERIKALI Inatambua mchango wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika kulinda haki na ustawi wa wafanyakazi ambao ni nguvu kazi ya Taifa, hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi amesema hayo alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Ridhiwani Kikwete wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi la WCF.
Katambi amesema kupitia WCF wafanyakazi wanaopata ajali au ugonjwa unaotokana na kazi zao wanapatiwa matibabu, fidia ya ulemavu, au pensheni kwa wale wanaopoteza uwezo wa kufanya kazi kabisa na hivyo kuwawezesha kuendelea na maisha yao bila kudhoofika kiuchumi.
“Jambo hili linaleta utulivu mahala pa kazi kwa kuliondoa jukumu la kulipa fidia kwa mwajiri hivyo kupunguza lawama na malalamiko”, amesema.
Waziri Katambi amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Menejimenti ya WCF ikiwemo kuweka misingi madhubuti katika usimamiaji wa sera, sheria, taratibu pamoja na menejimenti thabiti ya mifumo ya kifedha.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho cha siku mbili chini ya mwenyekiti wake ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma, kitajadili na kupitisha Mpango wa nane.