Na Lucy Lyatuu
WIZARA ya Afya imesema kwa mwaka wa fedha 2025/26, imetenga jumla ya Sh bilioni 13.6 ukilinganisha Sh bilioni 10.95 zilizotengwa mwaka wa fedha 2023/24 hivyo kufanya ongezeko la Sh bilioni 2.73 sawa na asilimia 25.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, Roida Andusamile azma ya Serikali ni kuongeza bajeti ya mafunzo ya wataalam bingwa na bobezi katika fani mbalimbali za Sekta ya afya kila inapowezekana.
Amesema Wizara ya Afya inawahimiza watumishi wote waliopata ufadhili kwa mwaka 2025/26 kukamilisha taratibu za kujaza mikataba ya ufadhili kama ishara ya kukubali ufadhili huu kabla au ifikapo Novemba 22, 2025.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 maombi ya ufadhili 1,074 yaliwasilishwa na kati ya hayo, waombaji 981 walikidhi vigezo vya kufadhiliwa na waliochaguliwa kwa ajili ya ufadhili kulingana na fedha iliyotengwa ni 498 sawa na asilimia 51 ya waombaji waliokidhi vigezo.
Amesema fedha iliyotengwa itatumika kufadhili watumishi wapya 498 pamoja na 985 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi na kufanya jumla ya watakaofadhiliwa kwa mwaka 2025/26 kuwa 1,483.
Aidha, kati ya watumishi 498 waliochaguliwa kupata ufadhili, watumishi 442 wamechaguliwa kupata ufadhili katika vyuo vikuu vya ndani ya nchi na 56 wamepata ufadhili katika vyuo vya nje ya nchi kwakuwa taaluma wanaozoenda kusoma hazipatikani katika vyuo vya ndani ya nchi.
Amesema Wizara imezingatia vipaumbele muhimu vya kisekta kama ubobezi katika ngazi mbalimbali za huduma Pamoja na vipaumbele kama vilivyoainishwa kwenye Mpango Mkakati wa Tano wa Sekta ya Afya pamoja na bajeti ya Serikali ya mwaka 2025/26.
Amevitaja vipaumbele hivyo ni Pamoja na taaluma za kuimarisha huduma za watoto, uzazi na magonjwa ya wanawake, saratani, magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama ya moyo na figo, matibabu ya ubongo na mishipa ya fahamu, afya ya akili, afya ya kinywa na meno, huduma mahsusi za upasuaji ikiwemo masikio, pua na koo, huduma za utengemao na tiba shufaa, ugunduzi wa magonjwa ikiwemo patholojia.
Amesema nakala ya mkataba inapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya afya na pia itatumwa kupitia anuani za barua pepe walizotumia wakati wa kuwasilisha maombi.
Nakala tatu (halisi) za mkataba zilizojazwa pamoja na barua za wadhamini ziwasilishwe katika ofisi ya Wizara ya Afya Makao Makuu, Mtumba Jijini Dodoma.
“ Ufadhili huu ni kwa ajili ya kulipiwa ada ya mafunzo na posho ya utafiti kwa watakaofadhiliwa ndani ya nchi,” amesema na kuongeza kuwa kwa wale watakaosoma vyuo vya nje ya nchi watalipiwa ada, posho ya kujikimu wakiwa masomoni, nauli ya kwenda na kurudi pamoja na posho ya utafiti.
Aidha amesema malipo ya posho ya utafiti na posho ya kujikimu yatazingatia viwango vilivyopangwa na Wizara.

