Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WATANZANIA wameshauri kula vyakula vya asili wakiwemo senene, kumbikumbi, msusa, ngogwe na vinginevyo ili kupata mlo kamili, kuepuka udumavu.
Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Chakula na Lishe, Dkt. Germana Leina amesema hayo wakati akichangia mada katika Kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na maonesho lililoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) lililomalizika hivi karibuni.
Katika kongamano hilo ametoa mchango unaohusiana na lishe katika mada iliyoeleza ni namna gani inaweza ikatumika elimu ya zamani, kimila au kitamaduni katika kutatua changamoto za lishe.
Amesema watanzania wakila vyakula hivyo vya asili vitasaidia kukidhi au kujaza pengo lililopo katika masuala ya lishe.
“Tafiti nyingi zinazofanywa zinazungumzia kwamba vyakula vya kitanzania huwa ni vya aina moja tu, yaani asilimia kubwa ya nishati lishe imetokana na kundi moja la vyakula ambavyo mara nyingi ni vile ambavyo vinatokana na nafaka mizizi na jamii ya ndizi mbichi, hivyo ni muhimu kutumia vyakula vya kizamani au vya kimili kama senene, kumbikumbi, msusa, ngogwe,” amesema.
Amesema wakishirikiana wanasayansi wa sasa pamoja na wale waliokuwa na ufahamu wa mila na tamaduni za makuzi ya chakula wanaweza wakaja na chakula ambacho kina lishe bora zaidi, kitakachokidhi mahitaji ya kilishe.
“Kama mnavyofahamu asilimia 30 ya watanzania wana udumavu, kwa bahati mbaya wengi wa hawa watoto wetu wako katika Kanda ambazo zinazalisha sana.
“Inawezekana kabisa chakula kinacholimwa ni cha aina moja tu na hivyo wakiweza kuongeza upatikanaji wa vyakula mbadala au vya kitamaduni tutaweza kuvuka hili pengo ambalo lipo la kilishe,” amesema.