Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: SERIKALI imeagiza kuwatumia wanasayansi wa ndani ya nchi badala ya kuwavunja moyo kwa kuwa wanafanya kazi nzuri ya kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Mkuu. Dkt. Dotto Biteko leo Disemba mbili, 2024 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kufungua Kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na maonesho linaloendelea Jijini Dar es Salaam.
Amesema, “Umefika wakati kwa Serikali, taasisi na Mashirika kutambua, kuthamini na kutumia tafiti za wanasayansi wa ndani ya nchi ili kutatua changamoto zilizopo,”.

DKt. Biteko amesema wanasayansi nchini wanafanya kazi nzuri na kubwa ya kutafuta suluhu ya matatizo mbalimbali katika jamii lakini kazi zao zinatambuliwa zaidi nje ya nchi kuliko zinavyotambuliwa nchini jambo ambalo linaweza kuwavunja moyo.
“Kongamano hilo ni la kujadili na kutafuta suluhu ya matatizo tuliyonayo, tutumie tafiti za wanasayansi wa ndani badala ya kuwavunja moyo na kila anayejaribu kwa kutafiti apewe fursa ili aendelee kutafiti zaidi na matokeo tutayaona,” amesema.
Biteko amesema kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), serikali imetoa sh Bilioni 32 kwa ajili ya kuimarisha miradi ya utafiti na ubunifu.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imeanza kutambua jitihada za Wanasayansi, Watafiti wa ndani ya nchi na baadhi yao wametunukiwa vyeti kwa kutambua mchango wao kwa maendeleo yaliyofikiwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo na uvuvi.
Amesema njia moja ya kufanya jitihada hizo kuwa endelevu, Serikali imeanzisha mfuko wa mikopo nafuu wa kubiasharisha bunifu na tafiti Tanzania unaojulikana kama ‘Samia Fund’.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu ameishukuru Serikali kwa uwezeshaji ambao umeiwezesha kutekeleza majukumu yake kwa viwango na kuwa moja ya taasisi mahiri ya kupigiwa mfano Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Amesema COSTECH kupitia program mbalimbali imewasaidia vijana wengi kubadili ndoto zao kuwa fursa ambapo pamoja na mambo mengine imefikia uwezo wa kutoa vibali 1000 kwa watafiti kutoka nje ya nchi.
Balozi wa Norway nchini, Tine Tonnes ameipongeza Tanzania kwa hatua zake za kuendeleza watafiti na wabunifu huku akieleza utayari wa nchi hiyo kuendelea kuunga mkono program za uhifadhi wa mazingira.