Baadhi ya vifaa maalumu ‘viona mbali’ kwa ajili ya ajili ya mafunzo ya elimu ya anga vilivyotumika katika mfumo ya utalii wa anga
Na Vincent Mpepo
ARUSHA: WATAALAMU wa elimu na utalii wametoa wito kwa mamlaka husika kulirejesha somo la Elimu ya Anga (Astronomia) katika mtaala wa shule za sekondari, ili kuwapata wataalamu zaidi watakaokuza sekta mpya ya utalii wa anga nchini.
Wito huo umetolewa na Mhadhiri Mwandamizi wa Fizikia na mtaalamu wa astronomia kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dkt. Noorali Jiwaji, wakati wa mafunzo ya biashara ya utalii wa anga yaliyofanyika mjini Karatu, mkoani Arusha.
“Nashangaa tutawapata wapi wanafunzi wenye msingi wa astronomia kama mtaala wa elimu wenyewe umelitupilia mbali somo hili muhimu,” amesema Dkt. Jiwaji.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya utalli wa anga wakifuatilia mafunzo hayo yaliyofanyika Karatu, Mkoani Arusha. (Picha na Vincent Mpepo).
Amesisitiza wakati Tanzania ikilenga kuanzisha utalii wa anga kama sekta mpya ya kiuchumi, ni muhimu elimu ya astronomia ikapewa kipaumbele kuanzia ngazi za chini za elimu.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa OUT mstaafu, Profesa Elifas Bisanda, ametoa rai kwa serikali kuanzisha somo la utalii wa anga kuanzia shule za msingi ili kuwaandaa mapema wataalamu wa baadaye.
“Utalii wa anga ni eneo jipya lenye fursa nyingi kwa nchi yetu. Ili kunufaika, tunahitaji kuanza mapema kuwaandaa wataalamu kupitia elimu rasmi,” amesema Bisanda.
Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo kujiunga na mtandao wa Anga-Giza (DarkSky – Tanzania) ili kukuza ushirikiano wa kitaalamu.
Naye Rais wa Chama cha Kimataifa cha Anga-Giza (International Dark-Sky Association) kutoka New Zealand, Nalayini Davis, amesema Tanzania ina nafasi ya kipekee katika kukuza utalii wa anga kutokana na mazingira bora ya asili, hali nzuri ya hewa na mandhari ya kuvutia.
“Ni wakati muafaka kwa Tanzania kuwekeza katika utalii wa anga kutokana na anga lenye giza safi na mandhari bora zinazotupa faida ambazo hazipaswi kupuuzwa,” amesema Davis.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na OUT, yakifadhiliwa na wataalamu kutoka New Zealand na Marekani, na yalihudhuriwa na wadau wa utalii wakiwemo waongoza watalii, watoa huduma za utalii, watunga sera, watafiti na wanataaluma zaidi ya 70.