Na Lucy Ngowi
MOROGORO: KATIKA kuhakikisha taifa linakuwa na wataalamu mahiri katika sekta ya ufundi stadi, serikali kupitia Chuo cha Ualimu na Ufundi Stadi Morogoro (MVTC) imepanua wigo wa utoaji wa mafunzo ya ualimu wa ufundi, huku dirisha la udahili kwa mwaka huu likiwa wazi hadi mwisho wa mwezi Septemba.
Akizungumza na vyombo vya habari, Mkufunzi Mwandamizi wa chuo hicho, Rodgers Sabuni, amesema chuo hicho ndicho pekee nchini kilichopewa dhamana ya kitaifa ya kuwaandaa walimu wa kufundisha vyuo vya ufundi stadi vya serikali na binafsi.
“Huwezi kuwa mwalimu wa ufundi bila kupita kwenye mafunzo ya ualimu,” amesema Sabuni na kufafanua kuwa mafunzo yanayotolewa yanazingatia mbinu bora za kufundisha kwa vitendo, sambamba na miongozo ya serikali kuhusu uboreshaji wa elimu ya ufundi.
Amesema MVTC kwa sasa inatoa kozi tatu kuu ambazo ni Astashahada ya Uzamili ya Ualimu wa Ufundi Stadi Kwa wahitimu wa shahada ya kwanza ya uhandisi.
“Hii huwaandaa kufundisha walimu wa vyuo vya ufundi,” amesema.
Pia Cheti cha Walimu Wasaidizi wa Ufundi Kwa wahitimu wa ngazi ya vyeti kutoka vyuo kama VETA, wanaopata mafunzo ya mwaka mmoja katika mbinu za kufundishia kwa vitendo, hasa katika fani za karakana.
Vile vile Diploma ya Ualimu wa Ufundi katika Uhandisi, kozi mpya zinazolenga kuandaa walimu wa ufundi kwa mahitaji mapana ya sasa ya kitaifa.
Katika jitihada za kuleta usawa na kuwafikia Watanzania wengi, Sabuni amesema kuwa chuo hicho hutoa elimu kwa njia mbili ya masafa na ya ana kwa ana ili kuwawezesha hata wale walioko mbali kupata fursa hiyo adhimu.
Sabuni amesema mabadiliko ya sera ya elimu yamefungua milango mipana ya ajira kwa walimu wa ufundi, kwani shule nyingi za sekondari zinaanzisha mchepuo wa masomo ya ufundi huku serikali ikiendelea kujenga vyuo vya VETA katika kila wilaya.
“Hii ni fursa ya kipekee kwa vijana waliomaliza kidato cha nne, vyuo vya ufundi au vyuo vikuu kujiunga na mafunzo haya ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza uchumi wa viwanda nchini,” amesema Sabuni.
Amesema kutokana na mahitaji makubwa ya walimu wa ufundi nchini, MVTC inatoa wito kwa vijana wote wenye nia ya kujihusisha na ualimu wa ufundi kuchangamkia dirisha la udahili lililofunguliwa kuanzia mwezi Juni hadi Septemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa Sabuni, wahitimu wa mafunzo hayo hupata nafasi kubwa ya ajira katika sekta ya elimu ya ufundi na teknolojia, sambamba na kuwa chachu ya maendeleo katika jamii zao.
“Tunaandaa walimu wa ufundi si kwa ajili ya vyuo vya VETA tu, bali pia kwa shule za sekondari zinazotekeleza mchepuo wa ufundi. Hii ni nafasi ya kipekee kwa vijana wetu kushiriki katika ujenzi wa taifa kupitia taaluma hii ya kipekee,” amehitimisha.