Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WANANCHI wa Jimbo la Kasulu Vijijini wanaendelea kunufaika na uwepo wa mwekezaji katika kitalu cha Makere Forest Reserve kupitia mgao wa fedha za maendeleo ya jamii, zaidi ya Sh. Milioni 12 kila mwaka, zinazotolewa na mwekezaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya vijiji.
Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, akijibu swali la Mbunge wa Jimbo hilo, Edibil Kazala Kinyoma, alipotaka kujua ni kwa kiasi gani wananchi wanapata faida kutokana na uwepo wa mwekezaji.
Dkt. Kijaji amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, vijiji vya Kagera Nkanda, Chekenya na Kabulanzwili vilipokea Sh. Milioni 4.4 kila kimoja.

Aidha, fedha zinazotokana na asilimia 25 ya ada ya wanyamapori wanaowindwa zinalipwa na Serikali kwa Halmashauri husika, kama inavyotolewa na Kifungu cha 137 cha Sheria ya Fedha ya Mwaka 2025.
Ameongeza kuwa asilimia 60 ya fedha hizi hutumika kutekeleza miradi ya maendeleo, huku asilimia 40 zikielekezwa katika shughuli za uhifadhi katika vijiji vinavyozunguka kitalu.
Sambamba na hayo, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26, mwekezaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) wamechangia miradi ya jamii yenye thamani ya Sh. Milioni 166.4.
Fedha hizo zimewezesha kufadhili kambi ya huduma ya matibabu ya macho katika Halmashauri ya Kasulu, ujenzi wa madawati 100 katika shule za msingi Chekenya (25), Nyakasanda (25) na Nyantuku (50),
Uchimbaji wa visima vya maji sita katika shule za msingi Kamganza, Kasasa, Mwitiri, Chekenya na Nyantuku, pamoja na kusaidia Kituo cha Afya cha Kagerankanda.

