Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), kinajadili na kuchambua masuala yanayogusa dini, utamaduni na siasa ili kujenga misingi ya maelewano, heshima na mshikamano katika jamii.
Mhadhiri Msaidizi kutoka Idara ya Falsafa na Taaluma za Dini, Valeri Mujuni amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa habari hizi katika banda la chuo hicho lililopo katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema pia katika maonesho hayo wanaeleza wananchi, kuhusu mradi huo unaolenga kuchochea mjadala wa kina kuhusu nafasi ya dini na utamaduni katika jamii ya sasa.
Amesema Mradi huo, unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), unalenga kufanya tafiti zinazochambua mitazamo tofauti kuhusu masuala ya kidini ambayo kwa muda mrefu hayajapewa utafiti wa kina, huku ukilenga kuibua majibu mbadala kwa changamoto zinazojitokeza katika jamii.
“Tumejikita katika kufanyia kazi maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa yakionekana kuwa nyeti, kama vile ukinzani kati ya dini na siasa. Tunafahamu kuwa kuna mstari mwembamba unaotenganisha maeneo haya, na kwa sababu hiyo tunahitaji uelewa wa pamoja,” amesema Mujuni.
Amesema Mradi huo umekuwa jukwaa la wazi kwa wanafunzi na wataalamu kutoka nyanja mbalimbali kushiriki katika mashauriano, kubadilishana mawazo na kushirikiana kwa lengo la kukuza uelewa wa kijamii na kukuza misingi ya haki za binadamu kupitia falsafa na tafakuri ya kidini.
“Tunatumia falsafa kama chombo cha kuchambua kwa undani haki ya binadamu na namna tunavyoweza kuishi kwa kuheshimiana, kupendana na kujaliana licha ya tofauti zetu za kidini au kitamaduni,” amesema.
Kupitia ushiriki wao katika maonesho ya Sabasaba, amesema kwamba wanatoa picha ya mchango mkubwa wa taaluma ya dini katika kutatua changamoto za kijamii, huku wakisisitiza umuhimu wa tafiti shirikishi na mjadala wa wazi katika kujenga jamii yenye mshikamano na maelewano ya kweli.