Mkurugenzi Wa Confucius Awakumbusha Wanafunzi Kujali Muda
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimewataka wanafunzi wa Kitanzania waliokwenda China, kuiwakilisha Tanzania kwa mambo mazuri, kuitangaza na kuelezea fursa za kiuchumi zilizopo.

Rasi wa Ndaki ya Insia, chuoni hapo Dkt Silkiluwasha Mpale aliwaasa wanafunzi 19 kutoka shule mbalimbali ambao wamekwenda China kwa ajili ya msimu wa hali ya joto, kuwakilisha nchi vizuri kwa siku zote watakazokuwepo huko.
Amesema, “Tusingependa kusikia kuna aliyeonekana kwenye kamera kwa kufanya udokozi au vitendo vyovyote vibaya,”.
Amesema wanafunzi waliopata fursa hiyo ni wale ambao shule zao zinafundisha lugha ya kichina, waliagwa katika Ukumbi wa Taasisi ya kufundisha lugha ya Kichina ya Confucius UDSM.
Amewakumbusha wanafunzi hao kuwa hawaendi peke yao bali wanawakilisha Tanzania,wazazi wao na Afrika kwa ujumla.
Pia amewataka wazazi wa wanafunzi hao, kuwaunga mkono watoto wanapotaka kusoma kichina kwani hata hao waliokwenda hawajaenda tu bali wameanza kujifunza kichina hivyo wanaenda huko kujifunza kwa kuona na vitendo.
“Nchi yetu ikiwa kwenye mageuzi ya elimu kwa kukazania zaidi masomo ya amali, hiki wanachoenda kujifunza watoto wetu huko China ndio kinamaanisha,
“Kwani enzi zetu kuna waliosoma kitabu cha ‘The great Wall of China’,lakini tuliishia kukiona kwenye vitabu na kuvuta picha kichwani tu, lakini leo hawa watoto wanaenda kuona kwa macho yao,” amesena.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Confucius upande wa China, Profesa Zhang Xiaozhen, amesema wanafunzi hao watakuwa nchini humo kwa wiki mbili.

Zhang amesema katika kipindi chote hicho watajifunza mambo mbalimbali ikiwemo lugha, tamaduni za kichina, shughuli mbalimbali zinazofanywa na nchi hiyo ikiwemo za kiuchumi na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.
Amewataka wanafunzi hao kuzingatia ratiba ya kila wanachopangiwa.
Kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Darren Samuel amesema wanashukuru kwa kupata nafasi hiyo kwa kuwa inawafungulia fursa nyingine katika maisha yao.

Amesema wakiwa nchini China watakuwa wawakilishi bora, kwa kuitambulisha vena Tanzania.