Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: HATIMAYE wanafunzi wawili wameibuka kidedea katika mashindano ya kuzungumza lugha ya Kichina, ‘ Chinese Bridge’ ambao watapata fursa ya kwenda nchini China kwa ajili ya fainali ya Kimataifa.
Mshindi maalum katika mashindano hayo ametoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kuluthum Maftah ambaye atashiriki mashindano yatakayofanyika nchini China, huku mshindi wa kwanza kutoka Chuo Kikuu Cha Waislam Morogoro (MUM), Sara mfinanga atapata nafasi ya kwenda kuyashuhudia.
Akizungumza wakati wa mashindano yaliyofanyika UDSM, Rasi wa Ndaki ya Insia, chuoni hapo Dkt. Silkiluwasha Mpale ambaye amemwakilisha Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema mashindano hayo ya ” Chinese Bridge yanahusisha vipaji mbalimbali kutoka kwa washiriki wake.

Amesema mashindano hayo ni ya 24 ya umahiri wa Lugha ya Kichina na ya 12 kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Tanzania.
Amesema lengo la mashindano hayo ni kuthamini ujuzi wa wanafunzi katika stadi mbalimbali za lugha ya kichina na tamaduni zake.
” Miongoni mwa maeneo yanayotazamwa ni utoaji wa hotuba, uimbaji wa nyimbo, kughani mashairi na Sanaa mbalimbali ikiwa ni pmoja na uchoraji,” amesema.

Pia amesema taasisi ya kufundisha lugha ya Kichina ya Confucius imeanza kutoa mafunzo ya lugha ya kiswahili kwa wachina wanaoishi nchini Tanzania.
“Wachina hawa wamependa kufundishwa na walimu wanaofahamu lugha na utamaduni wa Kichina. Kwa kufanya hivi tunakamilisha msemo wa nipe nikupe.
” Kwa maana kwamba sisi tunajifunza lugha na utamaduni wa Kichina, wakati huo huo wachina wanajifunza lugha na utamaduni wa Kiswahili,” amesema.
Mkurugenzi Mtanzania wa Confucius Dkt. Mussa Hans, amesema kwamba mashindano hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002 na hufanyika katika hatua mbili.

“Hatua ya kwanza hufanyika katika nchi mbalimbali ulimwenguni , hatua ya pili ni fainali ya kimataifa ambayo hufanyika nchini China.
” Hadi sasa zaidi ya wanafunzi milioni 1.5 kutoka zaidi ya nchi 150 wamekwishashiriki mashindano haya na kuonesha mafanikio makubwa katika kujifunza kwa kichina.
“Zaidi ya washindi 5000 wamekwishasafirishwa kwenda China kushiriki mashindano ya fainali ya kimataifa,” amesema.

Amesema lengo la mashindano hayo ni kutoa jukwaa kwa washiriki kutoka maeneo mbalimbali kuonesha ustadi wao wa lugha ya kichina, kujenga mtandao baina yao na kuhamasisha kufanya bidii zaidi katika kujifunza lugha na utamaduni wa kichina.
“Taasisi yetu ya Confucius pia imedhamiria kuwa daraja baina ya wahitimu wa mafunzo ya kichina na makampuni mbalimbali kwa lengo la kutafuta fursa mbalimbali,” amesema.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Balozi wa China nchini, Wang Yong amesema kushiriki kikamilifu katika shindano hilo kwa wanafunzi wa Kitanzania kunaonyesha nia, shauku na matarajio ya vyuo vya Tanzania, wazazi na wanafunzi katika kujifunza lugha hiyo na kuelewa utamaduni wake.
“Ubalozi wa China unatumai kuwa mashindano hayo yatakuwa faraja na jukwaa la kukuza ufundishaji na ujifunzaji wa Kichina nchini Tanzania,

“Pia kukuza mawasiliano ya kitamaduni baina ya nchi hizi mbili ” amesema.