Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 9

Wanafunzi 40 Babati Kuwa Mabalozi Wa Uhifadhi Vijijini

Na Mwandishi Wetu

BABATI: WANAFUNZI 40 wa shule za sekondari zilizopo katika eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge wilayani Babati, wametakiwa kutumia elimu waliyoipata kuhusu uhifadhi na mabadiliko ya tabianchi kuelimisha jamii za vijijini.

Wanafunzi hao wamepatiwa mafunzo ya vitendo kuhusu uhifadhi wa mazingira, utalii na wanyamapori kupitia ziara ya siku tano katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, iliyoandaliwa na taasisi ya Chem Chem Association.

Akizungumza Oktoba 25, 2026, alipowapokea wanafunzi hao baada ya kurejea Babati, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, amesema elimu hiyo inapaswa kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuongeza uelewa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kutunza mazingira.

Habari Picha 14203

Amesema Babati ni miongoni mwa maeneo yanayoathiriwa na mabadiliko hayo, huku baadhi ya wananchi wakiwa bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu athari zake.

“Misimu ya mvua imebadilika sana na joto limeongezeka. Ninyi mmepewa elimu kuhusu masuala haya, ikiwemo utunzaji wa mazingira. Tunatarajia mtakaporejea vijijini, mshirikiane na walimu wenu pamoja na wadau wengine kutoa elimu hiyo kwa jamii,” amesema Mbogo.

Ameongeza kuwa wanafunzi hao wamepata fursa muhimu ya kutembelea Serengeti na Ngorongoro kujifunza kwa vitendo, hivyo wanapaswa kuwa mabalozi wa uhifadhi na utalii katika maeneo yao.

Habari Picha 14204

Mkurugenzi wa Chem Chem Association, Clever Zulu, amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine imefadhili ziara hiyo kwa mara ya pili ili kuwajengea wanafunzi uelewa wa vitendo kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utalii.

“Tunawaamini ninyi kama kizazi kijacho. Mkifahamu vizuri faida za uhifadhi na utalii, mtaweza kuwaelimisha wengine na kurithisha vizazi vijavyo maarifa kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira na wanyamapori,” amesema Zulu.

Kwa upande wake, Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Babati, Christopher Laizer, amesema ziara hiyo imeongeza idadi ya mabalozi wa uhifadhi watakaosaidia kuelimisha wananchi kuhusu faida za kutunza wanyamapori na kuendeleza utalii.

Habari Picha 14202

Ofisa Miradi ya Maendeleo ya Jamii wa Chem Chem Association, Napendali Wazoeli, amewashukuru walimu, kampuni ya utalii ya Kanaga, taasisi ya Mkono kwa Mkono na Serikali kwa kushirikiana kufanikisha ziara hiyo.

Baadhi ya wanafunzi walioshiriki, Fatuma Shaban na Lulu John, wamesema wamejifunza mambo mbalimbali kuhusu uhifadhi, tabia za wanyamapori na mabadiliko ya tabianchi, na wameahidi kutumia maarifa hayo kuelimisha jamii.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.