Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: UFUNDISHAJI wa lugha ya kichina nchini Tanzania na Bara la Afrika umeongeza kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kiutamaduni kati ya China na bara hilo.
Mkurugenzi Mtanzania Taasisi ya Kichina ya Confucius Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Aldin Mutembei amesema hayo alipokuwa akifungua warsha ya walimu wa lugha ya kichina nchini Tanzania iliyofanyika UDSM.
Profesa Mutembei amesema ufundishaji huo unatokana na ukweli kuwa lugha ni chombo muhimu cha kukuza maelewano kwani watanzania na waafrika wengine wanapata uelewa wa kina wa utamaduni wa China, historia na mtazamo wa dunia ambao ni muhimu kwa ajili ya kuimarisha diplomasia na kukuza uhusiano wa kirafiki kati ya China na mataifa ya Afrika.

Amesema warsha hiyo itaamsha majadiliano, kubadilishana mawazo na kuimarisha dhamira ya kuendeleza elimu ya lugha ya kichina nchini Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya Confucious, Profesa Zhang Xiaozhen amesema katika warsha hiyo walimu wa kichina wanaofundisha lugha hiyo hapa nchini na wengine waliotoka nchini China wameshiriki.

Walimu hao wa kichina hapa nchini wanafundisha lugha hiyo chuoni UDSM, Chuo Kikuu Dodoma ( UDOM), Zanzibar na shule za msingi na sekondari mbalimbali nchini.