Na Mwandishi Wetu
DODOMA: WIZARA na Taasisi mbalimbalii zilizopo nchini zimeagizwa kuitumia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, zinapotaka kufanya mapitio au utafiti wa Sheria zao.
Kwa kuwa kutofanya hivyo ni kukiuka Sheria na taratibu kwani Tume hiyo imeundwa kwa kazi hiyo.
Waziri wa Katiba na Sheria Profesa Paramagamba Kabudi ametoa agizo hilo alipokuwa akipokea taarifa nane za utafiti uliofanywa na Tume hiyo,katika mkutano uliofanyika kwenye Ukumbi wa Wizara hiyo.
Profesa Kabudi ametoa agizo hilo kutokana na ombi la Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Winifrada Korosso kueleza kuwa moja ya changamoto inayoikumba Tume hiyo ni baadhi ya Taasisi na Wizara kupeleka mapendekezo ya Sheria pasipo kupitishia kwenye Tume hiyo na kufanyiwa utafiti wa kina.

Akizungumzia hilo, Kabudi ameeleza hasara inayoweza kuikumba serikali kwa kupokea mapendekezo yasiyopitia kwenye Tume ya Kurekebisha Sheria kuwa yanasababisha Sheria hizo kutodumu kwa muda mrefu.
” Kwa bahati nzuri Mwanasheria Mkuu wa serikali upo hapa napenda ifahamike kwamba wizara au Taasisi yeyote inayotaka kufanya maboresho au kutungwa kwa Sheria mpya ni lazima maboresho hayo yafanywe na Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kuwa huko ndiko kwenye wabobevu,” amesema.
Amesema sio sawa kwa serikali kushughulikia msaada wa Sheria ambao utadumu kwa muda mfupi na kuhitaji maboresho,, changamoto hiyo itaondoka endapo kila mmoja atafanya kazi yake.
Kwa upande mwingine ameipongeza tume hiyo kwa kazi nzuri inayoifanya ikiwa ni pamoja na kushirikiana na wizara yake
kutekeleza falsafa ya serikali.
Tume ya Kurekebisha Sheria ndio chombo chenye jukumu la kufanya mapitio na utafiti wa Sheria zote hapa nchini ili kuzifanya ziishi kwa muda mrefu.
.