Na Danson Kaikage
DODOMA: WAUMINI wa dini ya Kiislamu nchini wametakiwa kusimamia misingi ya upendo, ushirikiano sambamba na kusimamia amani ya nchi.
Katibu wa Sekretarieti Baraza la Ulamaa Taifa Sheikh Swed Twaibu Swed, ameeleza hayo kwa niaba ya Muft Mkuu wa Tanzania Abubakari Zuber wakati wa Ibada ya sherehe ya sikukuu ya Eid ul- Fitr iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Sheikh Swed amesema waumini wa dini hiyo wanatakiwa kutambua wanayo kazi kubwa ya kulinda amani ya nchi na kuliombea taifa ili kuendelee kuwepo kwa amani na utulivu.
Akizungumzia suala la Uchaguzi Mkuu, amesema ni wajibu wa kila mtanzania kuhakikisha anakuwa mlinzi na balozi mwema wa kuhubiri amani ya nchi hususani wakati uchaguzi.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu wa kuwachagua wabunge,madiwani na Rais kwa maana hiyo ni wajibu wa kila mtanzania kusimama imara kuhakikisha amani na utulivu vinatawala.
“Tusikubali kugawanyika kwa namna yoyote ile na badala yake tushikamane kwani Tanzania ni yetu na sisi ndio watanzania wenye jukumu la kuitunza Tanzania kwa ajili ya vizazi vijavyo,” amesema.

Kwa kwa upande wake Sheikh Lali Abdul’Azizi ,Imam Masjid Bilaly Area C Jijini Dodoma,amewataka waumini wa dini ya kiislamu kuitumia sikukuu hiyo kutafakari mambo makuu ambayo Mungu amewatendea.
Amewataka wasitumie sikukuu hiyo kufanya anasa au kutumia vyakula na vinywaji ambavyo Mungu ameviharamisha.
