Na Lucy Lyatuu
DAR ES SALAAM : HOSPITALI Ya Rufaa ya Temeke imesema kuna ongezeko la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza kutoka 9566 mwaka 2022/23 na kufikia wagonjwa 11,175 sawa na asilimia 14.4. Kwa mwaka 2023/24.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke
Sixtus Mapunda amesema hayo leo alipomuwakilisha Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwenye hafla ya makabidhiano ya jengo la kutolea huduma za kusafisha damu katika Hospitali hiyo.
Akizungumza, Mapunda pia amewataka wahudumu wa afya Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na magonjwa yasiyoambukiza huku jamii ikisisitizwa kuzingatia mtindo bora wa maisha .
Akitoa taarifa ya Hospitali hiyo Mganga Mkuu Dkt Joseph Kimaro amesema mwaka 2023/24 Hospitali ilipokea takribani wagonjwa 412 waliohitaji huduma za usafishaji damu ambao walipatiwa rufaa hivyo kuanzishwa kwa huduma hiyo kutasaidia kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mamlaka ya Bandari TPA Abeid Galus amesema TPA itaendelea kushiriki katika miradi mbalimbali ya kijamii ambapo kwa sasa imetoa Sh milioni 251.26 kwa ajili ya maboresho ya jengo hilo pamoja na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya sh Milioni 10.