Na Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa majumbani kutoka mikoa mbalimbali nchini pamoja na Waandishi wa Habari, wamejengewa uelewa juu ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Pia wamejengewa uwezo juu ya mapambano dhidi ya virusi UKIMWI.
Shirika la Kazi Duniani ( ILO), kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA) pamoja na Chama cha Wafanyakazi na Hifadhi, Majumbani, Huduma mbalimbali na Ushauri ( CHODAWU), wameendesha warsha hiyo kwa kada hizo.

Warsha hiyo imeendeshwa katika maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Taarifa iliyotolewa imeeleza Waratibu waliofanikisha na kuwezesha katika warsha hiyo ni Meneja wa Mradi kutoka ILO. Chiku Semfuko, Asteria Mathias kutoka CHODAWU, pamoja na Joseph Mukoji kutoka shirika la WoteSawa.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Usekelege Mpulla ndiye amekuwa Mgeni Rasmi akiambatana na Mkurugenzi wa ILO Afrika Mashariki, Caroline Mugalla na Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Rehema Rudanga.

Mpulla wakati akifungua warsha hiyo amewapongeza ILO kwa kuiandaa kwa wafanyakazi wa majumbani, ambayo itasaidia kubadili mitazamo ya jamii kuhusu kundi hilo muhimu.
Naye Mkurugenzi wa ILO, Carolline amesema kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo, ametoa wito kwa mafunzo ya namna hiyo kuhusisha pia waajiri wa wafanyakazi wa nyumbani, kwa wakati ujao.

