Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: WAFANYAKAZI wa majumbani wameiomba Serikali kukamilisha haraka mchakato wa kuridhia Mkataba Na. 189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), kwa kuwa ucheleweshwaji huo unaendelea kuwaumiza kwa kufanya kazi katika mazingira yasiyo na staha wala ulinzi wa kisheria.
Wakizungumza kwenye kikao kazi cha mafunzo ya utatuzi wa migogoro kilichofanyika mjini Morogoro, wafanyakazi hao walieleza kuwa wengi wao hawana mikataba rasmi ya kazi, wanakosa mapumziko, haki ya faragha, na kinga ya kisheria.
“Wafanyakazi wa majumbani tunatakiwa kutambua haki, stahiki pamoja na sheria za haki na wajibu,” amesema Desdelia Saimon kutoka Morogoro,.
Amesema kuchelewa kuridhiwa kwa mkataba huo kunawafanya waendelee kufanya kazi katika mazingira hatarishi.

Naye Nasra Selemani kutoka Dar es Salaam amesema mkataba huo ukiidhinishwa utafungua fursa nyingi kwa wafanyakazi wa majumbani.
“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia mkataba huu ili na sisi tutendewe haki kama wafanyakazi wengine,” amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wafanyakazi wa Majumbani Tanzania, Zanini Athuman, amesema mkataba huo unaweka wazi stahiki halali kwa kundi hilo, ikiwa ni pamoja na mapumziko ya kutosha na mazingira ya kuishi kwa heshima kwa wale wanaoishi kwa waajiri.
Amesema licha ya sheria za kitaifa kutambua kundi hilo, utekelezaji wake unakuwa mgumu kutokana na nyumba ya mtu binafsi kutotambulika kama eneo rasmi la kazi.
Katibu Mkuu wa CHODAWU, Said Wamba, amehimiza wafanyakazi wa majumbani kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili wawe na sauti ya pamoja katika kudai haki na stahiki zao.
“Tunajaribu kuwainua hawa wafanyakazi wa majumbani. Wapo chini mno na hili si jukumu la CHODAWU pekee, bali jamii nzima inapaswa kushiriki kuwaokoa,” amesema.
Kwa mujibu wa Wamba, wafanyakazi hao hufanya kazi kubwa na muhimu kwa waajiri wao na taifa kwa ujumla, lakini hawapati matunda ya jasho lao.
Pia Mratibu wa mradi wa ILO, Chiku Semfuko, amesema mafunzo hayo yatawawezesha wafanyakazi wa majumbani kufahamu mahali sahihi pa kupeleka migogoro yao na namna ya kupata utatuzi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CMA Tanzania Bara, Usekelege Mpulla, amesema tume imekwishaandaa mwongozo maalumu wa kushughulikia migogoro ya wafanyakazi wa majumbani pekee kwa lengo la kutafsiri matakwa ya kisheria na mkataba namba 189.
“Tumejipanga kuhakikisha haki za wafanyakazi wa majumbani zinatolewa kwa wakati, na mafunzo haya yatawajengea uwezo wasuluhishi kumaliza migogoro kwa haraka,” amesema.
Akifungua mafunzo hayo, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Kazi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Rehema Moyo amesisitiza kuwa CMA inapaswa kutoa kipaumbele kwa migogoro ya wafanyakazi wa majumbani kutokana na ugumu wa mazingira wanayopitia.
“Ni muhimu hata wao wafahamu haki zao. Hata kama vyombo vipo, lazima wapewe elimu ya kujua wapi waende kupata suluhu ya migogoro yao,” amesema Moyo.
Katika kuhakikisha haki za wafanyakazi wa majumbani zinalindwa ipasavyo, Shirika la Kazi Duniani (ILO) limewakutanisha mkoani Morogoro Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), taasisi zinazohusika na migogoro ya kazi, pamoja na wawakilishi wa wafanyakazi wa majumbani kwa lengo la kutafuta suluhu ya pamoja