Na Lucy Ngowi
DODOMA: BODI ya Mkonge Tanzania imewataka wadau mbalimbali kujiunga na mnyororo wa thamani wa mkonge, hususan katika eneo la uchakataji na uongezaji thamani wa zao hilo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka Bodi hiyo, Saimon Kibasa ametoa wito huo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma.
Amesema lengo ni kuwaelimisha wananchi na wawekezaji kuhusu fursa lukuki zilizopo katika sekta ya mkonge, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mbegu bora, utaalamu wa kilimo bora cha mkonge, na uwekezaji katika viwanda vya kuchakata zao hilo.
“Serikali ilianza rasmi kampeni ya kuhamasisha kilimo cha mkonge mwaka 2020, na tangu wakati huo, kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wakulima kote nchini.
“Kwa sasa, zao la mkonge limefikia hatua ya mwisho ya uzalishaji mashambani, na kinachohitajika sasa ni kuongeza uwezo wa kuchakata mkonge ili kuongeza thamani na tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla,” amesema.
Amesema Bodi hiyo inakaribisha wawekezaji kuanzisha au kuimarisha viwanda vya kuchakata mkonge, pamoja na kutoa huduma za kuchakata kwa wakulima wadogo, ili kuwawezesha kunufaika na zao hilo.
“Pia kuna fursa kubwa ya kuuza nyuzi za mkonge (singa) zinazozalishwa baada ya uchakataji, ambazo zina mahitaji makubwa katika masoko ya ndani na ya kimataifa, hasa kwenye viwanda vya kutengeneza kamba, mikeka, bidhaa za viwandani na hata nguo,” amesema.
Sekta ya mkonge inatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza kipato cha wakulima, kuboresha ajira vijijini, na kukuza pato la taifa, hivyo inahitaji ushiriki mpana kutoka kwa wadau wa sekta binafsi, taasisi za kifedha, na wajasiriamali.