Na Lucy Ngowi
GEITA: WACHIMBAJI wadogo wametakiwa kuachana na uchimbaji wa kubahatisha kwa kutumia teknolojia, taarifa sahihi za kijiolojia na vifaa bora ili kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama na kukuza mitaji yao.
Wito huo umetolewa na viongozi wa sekta ya madini wakati wa Maonesho ya tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Geita, wakizitaka kampuni kubwa za uchimbaji kushirikiana na wachimbaji wadogo kwa kuhamisha teknolojia na utaalamu.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji, John Bina na Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Dhahabu Taifa, Titus Kabuo, wamesema ushirikiano huo unaweza kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na kuwawezesha kukua hadi kuwa wachimbaji wakubwa.
Wamesema matumizi ya teknolojia za kisasa yanaweza kuboresha utafutaji, uchimbaji na uzalishaji wa madini, huku yakipunguza hasara zinazotokana na mbinu zisizo na tija.
Aidha, wameitaka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuimarisha upatikanaji wa taarifa za kijiolojia zinazoonesha maeneo yenye viashiria vya madini ili wachimbaji wafanye maamuzi kwa kuzingatia utafiti badala ya kubahatisha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wanawake Wachimbaji Mkoa wa Geita, Evelyn Nzinza, amesema upatikanaji wa vifaa bora kwa bei inayomudu wachimbaji ni muhimu kuongeza ufanisi wa uzalishaji.

Viongozi hao wamesema ushirikiano wa Serikali, taasisi za utafiti, kampuni kubwa na wachimbaji wadogo ni muhimu kuongeza tija, mapato na mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!