Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Ronald Lamola, amesema kuwa hali ya sasa ya siasa za dunia pamoja na vita vinavyoendelea katika Mashariki ya Kati imesababisha madhara makubwa kimataifa, ikiwemo kwa nchi za SADC.
Lamola pia ni Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, amesema hayo wakati akifungua mkutano wa 47 wa Baraza hilo unaofanyika jijini Pretoria, Afrika Kusini Machi 12 na 13, 2026.

Amesema hali hiyo ni ujumbe muhimu kwa nchi za ukanda huo kuchukua hatua madhubuti za pamoja ili kujinasua na athari hizo.
Akizungumza katika mkutano huo, Lamola amesema kuwa mivutano ya kisiasa na vita vinavyoendelea vinatishia uthabiti wa mnyororo wa biashara duniani.

Ameeleza kuwa kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la kimataifa kutaongeza gharama za uzalishaji wa mbolea, hali ambayo inaweza kusababisha kupanda kwa bei za vyakula.
Kwa mujibu wa Lamola, hali hiyo ni tishio kubwa kwa usalama wa chakula katika ukanda wa SADC, hasa ikizingatiwa kuwa takribani watu milioni 58 tayari wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula.

Aidha, ameeleza kuwa kutokana na hali ya vita katika Mashariki ya Kati, kuna uwezekano mkubwa kwa baadhi ya nchi za eneo hilo kupunguza au kusitisha mipango yao ya uwekezaji nje ya nchi na badala yake kuelekeza rasilimali katika masuala ya usalama wa ndani.
Ameonya kuwa hali hiyo inaweza kuwa na athari kubwa kwa ukanda wa SADC, hususan katika sekta za miundombinu, fedha, teknolojia, madini na nishati ambazo baadhi yake hutekelezwa kwa ushirikiano na nchi za Mashariki ya Kati.
Lamola pia amebainisha kuwa migogoro hiyo inaweza kupunguza juhudi za viongozi wa Afrika katika kutafuta suluhisho la tatizo la madeni kupitia majukwaa ya kimataifa.

Amesema kwa sasa nchi nyingi za Afrika hutumia fedha nyingi kulipa madeni, kiasi ambacho katika baadhi ya nchi huzidi hata bajeti za sekta za elimu na afya.
Kutokana na hali hiyo, amewataka mawaziri wanaoshiriki mkutano huo kutumia fursa hiyo kupanga mikakati madhubuti ya kukuza uchumi wa ukanda wa SADC, ambao bado unaendelea kukabiliana na athari za janga la COVID-19 pamoja na vita kati ya Urusi na Ukraine.

Katika mkutano huo, ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ngwaru Maghembe, akifuatana na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula.

