Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), CPA Beng’i Issa amewataka vijana kuweka akiba na kuacha tabia ya kutumia zaidi ya wanachokipata.
Beng’i ametoa rai hiyo Dar es Salaam, wakati akizindua Taasisi ya Chase Your Dreams, inayolenga kuwa mkono wa matumaini kwa vijana wa Kitanzania wanaopambana kufikia ndoto zao katika uchumi, elimu na ujasiriamali.
Amesema iwapo vijana wakizingatia uwekaji akiba na kutokutumia zaidi ya wanachopata, ni wazi kuwa watafanikiwa katika mipango yao, hivyo kutimiza ndoto zao.
“Ukipata elfu kumi, tumia elfu tano, Usitumie kupita kipato unachopata, la sivyo utakopa kwa ajili ya matumizi, wakati mikopo ni kwa ajili ya kuendeleza biashara ama uwekezaji”.
Katibu huyo amesema ujio wa Taasisi ya Chase unaleta hamasa mpya ya maendeleo ya vijana, hivyo ni imani yake baada ya miaka mitano kundi kubwa la vijana litakuwa limefikiwa.
Beng’i amesema Taifa la Tanzania linaweza kupiga hatua kubwa kupitia kundi la vijana, hivyo ofisi yake itaweka kipaumbele kwenye kundi hilo.
“Maendeleo ya taifa yanategemea vijana. Serikali iko tayari kushirikiana na taasisi kama hizi, ili kuhakikisha vijana wanatimiza malengo yao na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.”amesema.
Amesema mafanikio hayaji kwa bahati, bali kwa mpango, bidii na utekelezaji wa kile kinachowashinikiza ndani ya ndoto zao.
Kwa upande mwingine Beng’i amewataka vijana kujishughulisha na kuacha kukaa bure, kwani serikali imedhamiria kuwawezesha vijana, ikiwemo mpango wa kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana, kama ilivyotajwa katika hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassani wakati akifungua Bunge la 13.
Amewataka vijana wasiiogope dunia ya mafanikio, akiweka bayana kuwa maisha kuna kushindwa na kusonga mbele, hivyo wakifeli wainuke na wasiogope kufanya mambo makubwa.
Amefafanua kuwa uchumi ni nguzo muhimu katika heshima ya mtu kwenye jamii hata familia, kwa kuwa kukosa fedha huweza kumdhalilisha mtu kwenye ndoa, familia au katika mazingira ya kijamii.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Lightness Makondo, amesema Chase Your Dreams ilianzishwa kutokana na changamoto zinazowakabili vijana wa Kitanzania kwa kushindwa kufikia ndoto kutokana na ukosefu wa elimu sahihi, rasilimali na uongozi wa kitaaluma.
“Kila kijana ana ndoto ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii. Ndoto isipotekelezwa inabaki kuwa maono yasiyo na dira,”amesema.
Mkurugenzi huyo amesema Chase ni mwanga mpya kwa vijana wa Kitanzania. “Ni mwaliko wa kuamka, kuchukua hatua, kuweka mipango na kutumia fursa zilizopo ili kujenga maisha bora, uchumi imara na taifa lenye nguvu ya vijana. Ndoto hazijengwi kwa maneno zinajengwa kwa vitendo, nidhamu, mipango, na ujasiri” amesema.
Naye Joanitha Jeremiah kutoka Visionary Youth Organization amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa faida, ikiwemo kujifunza, kufanya biashara na kujenga mitandao ya maendeleo, badala ya kupoteza muda kwa malumbano, matusi na kuonyesha maisha ya kuigiza.
Wakili Fredric Usiku amewataka vijana kuacha woga kwani unachangia hasara kubwa sana. “Ukishindwa kufanya maamuzi, utashindwa kufika unapotaka,”amesema.

