Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ) Ridhiwani Kikwete amesema vijana ni chachu ya maendeleo endelevu wakiwezeshwa na kuwajibishwa kimazingira.
Amesema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa Vijana Wa Dunia katika Mji wa Suzhou, China.
Mkutano huo ambao hukutanisha vijana kutoka nchi mbalimbali duniani wakiwemo wanaotoka asasi za kiraia, mashirika ya kitaifa na kimataifa,na serikali mbalimbali ulibeba ujumbe unaosema Vijana ni Chachu ya Maendeleo Endelevu wapewe nafasi kuonyesha Uwepo wao.
Washiriki wa mkutano huo wametengeneza maazimio ambayo kila nchi iliyoshiriki itapaswa kuyaangalia ili kunyanyua ustawi wa vijana katika kushiriki ujenzi wa mataifa.
Mkutano huo ambao ulilenga pia kuangalia mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Malengo ya Millenia kwa upande wa vijana ulihudhuria na kuhutubia kwa njia ya mtandao moja kwa moja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Gilbert Houngbo na Mwakilishi Mkazi wa Shirika Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Idadi Ya watu duniani-(UNFPA) China Nadia Rasheed.
Kwa Pamoja washiriki hao walitoa msukumo kwa serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha wanatoa nafasi za kuwasikiliza na kuwahamasisha vijana kushiriki katika ujenzi wa sekta za maendeleo na kuwa wamoja katika kuyafikia malengo yao yakiwemo yale yanayowawezesha kuendelea.
Akihutubia Mkutano huo, Waziri Kikwete ameweka wazi hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa na serikali ya Awamu ya Sita ya Tanzania katika kuwawezesha vijana ikiwemo msisitizo mkubwa uliowekwa Kisera, kisheria na mipango mbalimbali ya kimaendeleo.
Pia Waziri huyo ameeleza na kuchambua vizuri hatua mbalimbali za mipango ya maendeleo na ushiriki wa vijana ikiwemo ile ya mgawanyo wa asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri, asilimia 30 za fedha za manunuzi ya umma,mikopo ya uwezeshaji wa umma ikiwemo ya NEEC, BEST.
Amesema pia zipo hatua za kushusha riba kwa wakopaji katika mabenki ya biashara, uundaji wa Sera mpya ya Vijana nchini, Programu za maendeleo kama BBT-Madini, Kilimo, Mifugo ambazo zimeonyesha mafanikio makubwa kwa sasa.
Mkutano huo ni wa 14 kukutanisha nchi wanachama na unafungua fursa kwa nchi wanachama , kukutana na kupeana uzoefu katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazokabili vijana Duniani.