Na Lucy Ngowi
MBEYA: Balozi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Kitengo cha Watu Wenye Mahitaji Maalum, Francis Anthony, amesema anachukia kuonavwenye mahitaji maalum wakiwa ombaomba hivyo anawahamasisha kujifunza ujuzi mbalimbali utakaowasaidia katika maisha yao.
Anthony amesema hayo mbele ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Mary Maganga, alipotembelea banda la VETA katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mkoani Mbeya.

Akimwelezea Katibu Mkuu huyo, Maganga amesema kwamba ni mhitimu wa VETA, fundi wa kompyuta aliyehitimu mafunzo ya kitaalamu na sasa anafundisha wengine.
Amesema uwepo wake katika maadhimisho hayo ni kuhamasisha vijana wenye ulemavu wasikate tamaa bali wajitokeze kupata mafunzo ya ufundi ili waweze kujitegemea kama wenzao.
“Nilianza kama mwanafunzi, sasa ninafundisha. Huu ni uthibitisho kuwa VETA imewajengea uwezo vijana wenye mahitaji maalum, na hata sisi tuna ujuzi wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” amesema.

Kwa upande wake, Riziki Ndumba, mwanafunzi wa VETA Songea anayesomea fani ya ushonaji, amesema alianza bila kuwa na ujuzi wowote wa awali, lakini kupitia mafunzo aliyopata na msaada kutoka kwa walimu pamoja na viongozi wa chuo, ameweza kumaliza kozi ya miaka miwili kwa mafanikio.
“Lengo langu ni kuonyesha kwa vitendo kuwa hata sisi wenye ulemavu tunaweza kufanya kazi na kujitegemea kama vijana wengine. Nawashukuru VETA kwa kutuamini na kutuwezesha,” amesema.

Naye Ofisa Uhusiano kwa Umma VETA Makao Makuu, Elmer Sarao, ameeleza kuwa taasisi hiyo inaendelea kutoa nafasi kwa vijana wenye ulemavu katika vyuo vyake.
Amesema mmoja wa walimu waliopo sasa ni mhitimu mwenye ulemavu aliyesoma VETA kuanzia mwaka wa kwanza hadi wa tatu, na sasa anafundisha katika chuo cha mafunzo stadi kilichopo Morogoro.
“Huyu ni mfano hai kuwa ulemavu si kikwazo cha ufanisi. Tunajivunia kuwalea na kuwaendeleza vijana hawa,” amesema.
Amesema VETA imekuwa ikitoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana wa makundi yote, ikiwemo wenye mahitaji maalum, kama sehemu ya juhudi za serikali katika kujenga taifa lenye nguvu kazi mahiri na jumuishi.