Na Lucy Ngowi
GEITA: CHUO cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Chang’ombe, Dar es Salaam, kimeonyesha mashine ya kisasa ya kukaushia samaki inayotumia umeme badala ya kuni au mkaa, ikiwa na uwezo wa kuchakata hadi kilo 500 na kusaidia kuongeza muda wa bidhaa hizo kukaa bila kuharibika.
Mashine hiyo imeonyeshwa katika Maonyesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Geita, ambapo VETA inashiriki kuonyesha teknolojia na ubunifu unaoweza kutumika katika shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Mwalimu wa VETA Chang’ombe mkoani Dar es Salaam, Emmanuel Bukuku, amesema mashine hiyo imezingatia mahitaji ya maeneo yenye shughuli za uvuvi, ikiwamo Kanda ya Ziwa, ambako samaki ni miongoni mwa bidhaa muhimu zinazozalishwa na wananchi.

Amesema teknolojia hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa katika ukaushaji wa samaki, huku ikisaidia bidhaa hizo kukauka kwa muda mfupi na kuhifadhi ubora wake.
“Faida ya mashine hii ni kwamba samaki wanakauka kwa muda mfupi, hawapotezi ladha yao na baada ya kukaushwa wanaweza kukaa muda mrefu bila kuharibika,” amesema Bukuku.
Amesema mashine hiyo pia inaweza kusaidia kupunguza utegemezi wa barafu katika kuhifadhi samaki wakati wa kusafirisha bidhaa hizo umbali mrefu.

Kwa mujibu wa Bukuku, teknolojia hiyo si kwa ajili ya samaki pekee, bali inaweza kutumika kukaushia dagaa, nyama na matunda kwa kuondoa unyevunyevu na kuongeza muda wa bidhaa hizo kukaa bila kuharibika.
Amesema VETA inaweza kutengeneza mashine hizo kwa ukubwa tofauti kulingana na mahitaji ya mteja, huku mashine inayoonyeshwa katika maonyesho hayo ikiwa na uwezo wa kuchakata hadi kilo 500.
“Tunatengeneza mashine kwa ukubwa tofauti kulingana na mahitaji ya mteja. Tunatarajia teknolojia hii itawasaidia wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine yanayofanya shughuli za uvuvi,” amesema.
Amesema bidhaa zilizokaushwa kwa mashine hiyo zinaweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu iwapo zitawekwa katika mazingira yanayofaa na yasiyo na unyevunyevu.

Maoni 0
Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!