Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imepanga kuimarisha ushirikiano na Toyota Tanzania Limited kwa ajili ya kuboresha mafunzo ya ufundi magari kwa wakufunzi na wanafunzi wa vyuo vya VETA.
Hayo yameelezwa katika ziara ya Menejimenti ya VETA ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Anthony Kasore, iliyoambatana na wataalam kutoka Makao Makuu ya VETA, Kanda ya Dar es Salaam, Chuo cha VETA Dar es Salaam na walimu wa vyuo vya Dar es Salaam na Pwani, iliyofanyika Agosti 12, mwaka huu 2025 katika ofisi na karakana za Toyota Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Kasore amesema lengo la ziara ni kujifunza kuhusu teknolojia mpya, mifumo ya matengenezo ya magari ya Toyota na namna kampuni hiyo inavyowawezesha mafundi kuwa mahiri.
Amesema VETA inakusudia kushirikiana na Toyota kutoa mafunzo ya kuongeza umahiri kwa wakufunzi na wanafunzi wa fani za magari.
“Magari ya Toyota yanatumika kwa kiwango kikubwa nchini, hivyo ni muhimu wakufunzi na wanafunzi wetu wawe na uelewa wa kina ili wafanye matengenezo bora,” amesema.
Meneja Mkuu wa Toyota Tanzania, Kadiva William, amepongeza hatua hiyo akisema, “VETA mnazalisha tunachokitumia, na sisi tunatoa huduma mnayoitumia, hivyo tunategemeana.”
Mkuu wa Shughuli za Usambazaji wa Toyota, Stanley Joseph, amesema ushirikiano huo utarahisisha utoaji wa mrejesho kuhusu wahitimu wa VETA na kufuatilia mabadiliko ya teknolojia, yakiwemo magari yanayotumia gesi na mafuta.

Mkufunzi wa Toyota, Michael Mruma, amesema kampuni hiyo ina chuo maalum kinachotoa mafunzo ya umakenika, umeme wa magari, urekebishaji bodi, huduma kwa wateja, usimamizi wa vifaa na mbinu za Kaizen. Ametoa wito wa kuunganisha mafunzo ya umakenika na umeme wa magari badala ya kuyatenganisha kama ilivyo sasa katika vyuo vya VETA.
Pande zote zimekubaliana kurasimisha ushirikiano ili kuhakikisha mafunzo yanalingana na mahitaji ya soko la ajira na kuinua viwango vya wakufunzi.
Kasore amesema VETA itaandaa andiko la mapendekezo ya kurasimisha ushirikiano huo.
Toyota kwa sasa inatoa nafasi za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa VETA katika vituo vya Dar es Salaam, Tanga na Arusha.