Na Danson Kaijage
Dodoma: MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa yamechochea mageuzi makubwa katika sekta ya uvuvi mkoani humo, na kuifanya Mwanza kuwa kinara katika uchakataji, usafirishaji na ufugaji wa samaki nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mtanda amesema mkoa huo umevuna matunda ya uwekezaji katika teknolojia ya uzalishaji na usindikaji wa mazao ya samaki, hatua inayochochea uchumi wa buluu na kuwanufaisha wananchi moja kwa moja.

“Idadi ya vizimba vya kufugia samaki imeongezeka kutoka 1,664 mwaka 2020 hadi kufikia 2,715 mwaka 2025. Ni mafanikio makubwa ya uwekezaji katika teknolojia ya kisasa ya ufugaji wa samaki,” amesema.
Kwa mujibu wa Mtanda, mwaka 2024 pekee zaidi ya tani 43,657.6 za minofu ya samaki zilichakatwa, huku tani 81,812 zikisafirishwa nje ya nchi kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwanza.
Pia, usafirishaji wa mabondo ya samaki nje ya nchi umeongezeka kutoka kilo 431,721 mwaka 2020 hadi kilo 495,448 mwaka 2024.

Amesema Idadi ya mabwawa ya kufugia samaki pia imepanda kutoka 286 mwaka 2020 hadi 531 mwaka 2025, ongezeko la zaidi ya asilimia 85.
“Mapato ya shughuli za uvuvi mkoani Mwanza yameongezeka kutoka Sh. Bilioni 4.4 mwaka 2020 hadi Bilioni 8.2 mwaka 2025.
“Haya ni mafanikio ya moja kwa moja ya sera na msukumo wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kukuza uchumi wa buluu,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema Mwanza itaendelea kuhamasisha uwekezaji, utafiti na matumizi ya teknolojia, ili kuhakikisha kuwa rasilimali za Ziwa Victoria zinawanufaisha wavuvi wadogo, wanawake, vijana na wafanyabiashara wa dagaa kwa uendelevu.