Na Mwandishi Wetu,
Antananarivo: MKUTANO wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimishwa jijini Antananarivo, Madagascar, Agosti 17, mwaka huu 2025, viongozi wakisisitiza umuhimu wa umoja, mshikamano na ushirikiano kama nyenzo kuu za maendeleo,
Ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazolikumba Bara la Afrika.

Tqarifa imesema katika mkutano huo, Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha Uenyekiti wa jumuiya hiyo ulikabidhiwa rasmi kwa Madagascar kutoka kwa Zimbabwe.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, Mkutano huo ulihudhuriwa na wakuu wa nchi tisa, huku wakuu wa nchi wa Botswana, Namibia, Msumbiji na Mauritius wakihutubia kwa mara ya kwanza tangu wachukue madaraka.

Viongozi hao waligusia kwa kina masuala ya amani na usalama, ujenzi wa miundombinu, ukuaji wa uchumi, demokrasia na mtangamano wa kikanda.
Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, ambaye alikamilisha kipindi chake cha uenyekiti, ameeleza kuwa hali ya kisiasa katika ukanda wa SADC ni ya kuridhisha, isipokuwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambako bado kuna changamoto za kiusalama.
Amesisitiza kuwa migogoro inayoibuka barani Afrika inapaswa kutatuliwa na Waafrika wenyewe, huku akieleza kuwa msaada wa nje unapaswa kuwa wa hiari na wa ziada tu.

Pia Viongozi wa SADC wamesisitiza umuhimu wa kukuza viwanda, kilimo, biashara na uongezaji thamani wa malighafi za ndani kama njia ya kuimarisha uchumi, kuongeza ajira na kipato hasa kwa vijana na wanawake.
Naye Rais wa Botswana, Duma Boko amesisitiza kuwa biashara baina ya nchi za Afrika ni njia madhubuti ya kujitegemea kiuchumi.
Katika eneo la miundombinu, nchi wanachama zilitakiwa kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara, reli, nishati, maji na TEHAMA, ambayo imeainishwa katika Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kikanda wa mwaka 2030.
Vile vile nchi tisa, zikiwemo Tanzania, tayari zimesaini itifaki ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda kwa ajili ya kugharamia miradi hiyo.
Mkutano huo ulitoa wito kwa nchi wanachama kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kuhakikisha kuwa Uchaguzi Mkuu katika nchi mbalimbali unaendeshwa kwa misingi ya haki, uhuru na uwazi.
Imesisitizwa pia kuimarisha Misheni ya Uangalizi ya Uchaguzi ya SADC ili kusaidia kulinda misingi ya demokrasia.
Viongozi wa SADC walihimiza kuondolewa kwa vikwazo vinavyokwamisha muingiliano wa watu na biashara baina ya nchi wanachama, ikiwemo masharti ya viza na vikwazo visivyo vya kiforodha. Lengo ni kuimarisha mtangamano na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika ukanda huo.