Na Danson Kaijage
TAASISI ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) zimeagizwa kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na kumsimamia Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ili mradi huo ukamilike kwa wakati na ubora.
Maelezo hayo yametolewa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika Jiji la Dodoma.
Ulega ameelekeza Taasisi hizo kuwa na mawasiliano na ushirikiano wa karibu kwani Watanzania wanasubiria mradi huo na kuahidi kuukagua mradi huo mara kwa mara.

Ulega amesema mradi huo uliofikia asilimia 53.9 ukikamilika utainua uchumi wa Mkoa wa Dodoma na kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji.
“Nimekagua jengo hili la abiria ambalo ni la kisasa na Mkandarasi yupo nyuma ya muda, hivyo nimeagiza Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group na Hebei Construction Group Corporation (BCEG) afanye kazi usiku na mchana na kuongeza idadi ya wafanyakazi,” amesema Ulega.
Ameongeza kuwa Serikali haitaongeza muda kwa Mkandarasi huyo kama atashindwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa wakati na atapaswa kuilipa Serikali fidia kwa kuchelewesha mradi.
“Nimetoa maelekezo kwa miradi yote Makandarasi wanapochelewesha miradi ambayo tuna uhakika tunayo fedha lazima tuwadai fidia,” amesema.
Waziri Ulega ameridhishwa na hatua za ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambayo imefikia asilimia 89 na kupongeza TANROADS na Mkandarasi Sinohydro kwa hatua hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuufungua mkoa huo kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa kiwanja hicho ambapo amesema uwepo wake ni fursa ya kijamii na kiuchumi kwa wana Dodoma na nchi kwa ujumla.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo amesema wanatarajia kuanza majaribio ya kuruhusu urukaji na utuaji wa ndege katika kiwanja hicho ifikapo mwezi Juni, 2025.