Na Danson Kaijage
DODOMA: UKUSANYAJI mapato katika Halmashauri hauridhishi hivyo zimeagizwa kuongeza juhudi katika ukusanyaji utokanao na majengo, mabango na shughuli nyingine.
Naibu Waziri wa TAMISEMI Dkt.Festo Ndugange, amesema hayo alipokuwa akifunga Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT)
kwa niaba ya Waziri Mohammed Mchengerwa uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano Jakaya Kikwete Jijini Dodoma .
Amesema, ” Halmashauri nyingi bado hazijafikia malengo ya ulusanyaji wa mapato kwani ni asilimia 38 tu zinazokusanywa hivyo kufanya mapato kwenye halmashauri kushuka,”.
Amesema wakati kodi za majengo na mabando zilipokuwa zikikusanywa na Serikali kuu yaani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), halmashauri nyingi zilipiga kelele kwa kueleza kuwa hazina mapato lakini baada ya kodi hizo kurudishwa halmashauri bado ukusanyaji wake unasuasua.
Amesema kitendo cha halmashauri kushindwa kukusanya mapato na kushindwa kufikisha lengo ni kipimo tosha kwa mkurugenzi husika kuwa hatoshi katika nafasi hiyo.
Pia amesema katika ukusanyaji wa mapato na utafutaji wa vyanzo vipya vya mapato ni vizuri kuwashirikisha wananchi wa sehemu husika ili kuepukana na migogoro pale inapoonekana kuna sehemu mpya inayoweza kusababisha mapato mapya ya halmashauri.
Katika eneo lingine ambalo amesisitiza ni suala la afya na kutoa maelekezo kuwa kila kituo cha Afya, Zahanati na Hospitali ni lazima ziwe na dawa muhimu za binadamu ili kuondoa malalamiko kwa wateja wanaotaka huduma hiyo.
Kwa upande wa elimu amezitaka halmashauri zote kuhakikisha wanapambana na mdondoko wa wanafunzi na kusimamia kila mtoto mwenye sifa ya kwenda shule aende asiishie njiani.
Amesema kila mwanafunzi kuanzia ngazi ya chekechea hadi kidato cha kwanza mwenye sifa ya kuwa shuleni aende shuleni na asikomee njiani.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa ,Costanine Simma amesema kuwa maagizo yote yaliyotolewa yatatekelezwa na kufanyiwa kazi kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.