Na Lucy Ngowi
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeendelea kuunganisha maarifa na maendeleo ya taifa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961, huku ushirikiano na China ukiwa sehemu muhimu ya mkakati wake wa maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye, Mkurugenzi wa Utafiti na Machapisho chuoni hapo, Dkt. Mathew Senga, amesema,
Tangu kuanzishwa kwa Taasisi ya Confucius mwaka 2013 kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Zhejiang Normal, taasisi hiyo imefanikiwa kuwafundisha karibu wanafunzi 60,000 lugha ya Kichina.
Dkt. Senga ameyasema hayo wakati wa Hafla ya Uchangiaji wa Vitabu katika Shubaka la Machapisho ya Kichina iliyoandaliwa chuoni hapo.
Amesema juhudi hizo zimefanikisha ujumuishaji wa lugha ya Kichina katika mfumo wa elimu wa taifa la Tanzania.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yameifanya Taasisi ya Confucius ya UDSM, iliyotunukiwa Tuzo ya Taasisi ya Confucius ya Mwaka 2017, kuwa mfano bora wa ushirikiano wa elimu kati ya China na Tanzania.
Akizungumzia Shubaka la Machapisho ya Kichina, Dkt. Senga amesema kuwa mpango huo utafungua dirisha jipya kwa wanafunzi wa Dar es Salaam kuielewa China kwa undani zaidi kupitia vitabu vinavyoelezea historia, maendeleo na falsafa ya taifa hilo.
“Hapa wanafunzi wataweza kuchunguza siri za maendeleo ya China kupitia vitabu, huku wakikusanya maarifa yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika ushirikiano wa baadaye kati ya China na Tanzania,” amesema.
Ameongeza kuwa vitabu hivyo, vilivyojaa maarifa na hekima, vitachukua mizizi na kuchipua kama mbegu, vikilea mabalozi wengi zaidi wa kuendeleza urafiki wa kudumu kati ya mataifa hayo mawili.
Kwa upande wake, Naibu Meneja Mkuu wa Kampuni ya China Communications Construction Company (CCCC) – Tawi la Tanzania, Deng Honglong, amesema hafla hiyo ni ya tatu mfululizo kuandaliwa kwa pamoja kati ya CCCC Tanzania na Taasisi ya Confucius.
Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, mpango huo umechangia kutoa vitabu vya lugha ya Kichina na Kiingereza kwa UDSM, vikihusisha fani mbalimbali zikiwemo tiba, fasihi, historia, sayansi na teknolojia pamoja na menejimenti.
“Kupitia vitabu hivi, hatuenezi maarifa pekee bali pia tunajenga madaraja ya urafiki kati ya China na Tanzania, huku tukiimarisha ushirikiano wa kielimu na kitamaduni,” amesema Deng.
Ameongeza kuwa kila kitabu kinabeba dhamira ya kuchangia ukuaji wa vijana wa Tanzania na kudumisha urafiki wa kudumu kati ya mataifa hayo mawili.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maktaba Kuu ya UDSM, Collin Kimaryo, amesema ushirikiano huo umeimarisha rasilimali za kitaaluma na kuendeleza mahusiano ya kitamaduni kati ya Tanzania na China.
Amesema jumla ya vitabu takribani 300 vimetolewa, vikihusisha fani za fasihi, sanaa na utamaduni, menejimenti, tiba, teknolojia, uhandisi na usanifu, kwa lugha za Kichina na Kiingereza.
Kwa mujibu wake, vitabu hivyo vitawanufaisha zaidi ya wanafunzi 20,000 na wahadhiri, katika masomo, utafiti na maendeleo ya taifa. Ameahidi kuwa maktaba itavihifadhi, kuvipanga vizuri na kuhakikisha vinapatikana kwa urahisi kwa watumiaji.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtanzania wa Taasisi ya Confucius, Dkt. Musa Hans, amesema hafla hiyo ni sehemu ya juhudi za pamoja kati ya Taasisi ya Confucius na CCCC Tanzania katika kuimarisha upatikanaji wa machapisho yanayoihusu China.
Amesema mchango wa mwaka huu una umuhimu wa kipekee kutokana na kuongezeka kwa idadi na mawanda ya machapisho ikilinganishwa na awamu zilizopita.
“Kupanuka kwa machapisho katika fani mbalimbali kunawapa wasomaji fursa ya kuielewa China kwa undani zaidi na kuona mnyororo wa mafanikio ya taifa hili ambalo linaendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo kila siku,” amesema.

