Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa William Anangisye, amesema utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET) umefikia zaidi ya asilimia 80, na umeleta mageuzi makubwa katika miundombinu, mitaala, na teknolojia ya kufundishia chuoni hapo.
Profesa Anangisye amesema hayo alipokuwa akielezea kwa Wahariri na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Amesema chuo hicho ilitengwa dola milioni 49.5 (takribani Sh bilioni 121) kati ya dola milioni 425 zilizotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.
Pia amesema kupitia mradi huo, UDSM imejenga kampasi mpya katika mikoa ya Lindi na Kagera, majengo 11 mapya ya kufundishia na ofisi za wahadhiri, pamoja na hosteli za wanafunzi. Pia, miundombinu ya TEHAMA imeimarishwa, na sasa chuo kina uwezo wa kusambaza mtandao wa hadi 10Mbps kutoka 1.5Mbps.
Profesa Anangisye amesema zaidi ya mitaala 250 imeboreshwa ili kuendana na soko la ajira, na masomo 1,000 yamewekwa katika mfumo wa kujifunza kwa njia ya mtandao unaowawezesha wanafunzi 39,000, wakiwemo 165 wenye mahitaji maalum.

Katika kukuza utafiti na ubunifu, UDSM imesaini mikataba ya ushirikiano na kampuni 24 za sekta binafsi, jambo lililosaidia wahitimu kupata uzoefu wa kazi na kuongeza ajira.
Aidha, wanataaluma 29 wamefadhiliwa kusoma nje ya nchi, wakiwemo wanawake 13, katika shahada za Uzamili na Uzamivu, ili kuongeza ubora wa ufundishaji na utafiti.
Profesa Anangisye amesema mafanikio ya HEET yameongeza ubora wa elimu, ubunifu, ajira kwa wahitimu, na kuifanya UDSM kuwa kinara wa mageuzi ya kidijitali katika elimu ya juu nchini.
Ametoa shukrani kwa Serikali , Wizara ya Elimu, na Benki ya Dunia kwa kusaidia kufanikisha mradi huo.
“HEET ni ukurasa mpya katika historia ya elimu ya juu nchini. UDSM itaendelea kuwa chachu ya maendeleo kupitia falsafa yake — Hekima ni Uhuru.”

Naye Naibu Mratibu wa HEET chuoni hapo, Profesa Liberato Haule amesema kupitia mradi huo wamefanikiwa kuboresha miundombinu ya ufundishaji ikiwemo ujenzi wa majengo mapya, madarasa na maabara za kisasa.
Amesema mradi huo pia umeweka kipaumbele kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kununua vifaa maalum vitakavyowawezesha kujifunza kwa urahisi pamoja na kurahisisha ufundishaji kwa walimu.

Kwa upande wa mageuzi ya mitaala, Profesa Haule anesema chuo kimepitisha mitaala 250 kupitia Seneti yake, ambapo 94 kati ya hiyo inatumika kupima matokeo ya mradi. Aidha, mitaala 32 imepata ithibati ya vyuo vikuu, miwili inatolewa kwa njia ya mtandao na 96 kwa mfumo wa mseto.
“Mabadiliko haya yanajibu kilio cha wadau wengi wanaotaka wahitimu wawe na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira,” amesema Profesa Haule.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amepongeza serikali kwa kufadhili mradi huo na kuwashukuru wasimamizi kwa utekelezaji mzuri.
Amesema waandishi wa habari wataendelea kutangaza ubunifu na mafanikio ya UDSM ili kuvutia wawekezaji zaidi katika sekta ya elimu ya juu.
