Na Lucy Ngowi
DODOMA: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM), kimeibuka na teknolojia mpya inayolenga kusaidia wafugaji wa samaki kwa kutumia mfumo wa kuhesabu samaki kwa njia ya kiotomatiki.
Mtaalamu wa maabara kutoka UDSM, Ditram Ngairo ameeleza hayo katika maonesho ya nanenane ya Kitaifa na Kimataifa yanayoendelea mkoani Dodoma.

Amesema katika ufugaji wa samaki kuna mambo makuu matatu yanayopaswa kuzingatiwa ikiwemo mazingira ya samaki ambayo ni maji na eneo la kufugia kama bwawa au vizimba, afya na ustawi wa samaki, pamoja na biashara ya samaki kati ya mfugaji na mnunuzi.

Amesema changamoto kubwa imekuwa ni namna ya kuhesabu idadi ya samaki kwa usahihi. Wafugaji wengi wamekuwa wakitumia njia za kupima au kuhesabu kwa mikono, ambazo zimekuwa zikichukua muda mrefu, kusababisha vifo vya samaki, na kuwapa samaki msongo wa mawazo ambao huathiri ukuaji wao.
Kwa kutambua tatizo hilo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia kwa watafiti wake kimebuni mfumo wa kuhesabu samaki kwa njia ya kiotomatiki.

“Mfumo huu unapunguza muda wa kuhesabu, hupunguza vifo vya samaki, na huongeza ufanisi wa uzalishaji,” amesema.
Amesema teknolojia hiyo haijawahi kutumika nchini Tanzania, na chuo kinaionesha katika maonesho hayo ya Nanenane mwaka huu 2025.
Wafugaji wa samaki wanahimizwa kutembelea banda la UDSM ili kujionea kwa vitendo namna mfumo huo unavyofanya kazi.