Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: WANANCHI wanaoishi Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam, wameiomba serikali kutatua changamoto ya usafiri inayowakabili katika kituo kilichopo Bunju Sokoni Dar es Salaam.
Kwa muda mrefu sasa wananchi wanaotumia barabara ya Bagamoyo kuelekea Bunju Sokoni wamekuwa hawana uhakika wa usafiri majira ya asubuhi wala kituo rasmi cha kupandia daladala kutokana na madereva kugomea kituo cha Bunju Sokoni kwa ajili ya kuharibika kipindi cha mvua.
Mwandishi wa habari hii mara kadhaa amekuwa akishuhudia kadhia wanayoipata wananchi katika kituo hicho ikiwemo ya daladala kufika na kulipa ushuru inayopokelewa na Halmashauri ya Kinondoni, kisha kuondoka bila kuchukua abiria.
“Kiukweli kituo hiki bora kisingekuwepo maana wananchi tumetelekezwa na serikali, lakini daladala zinazopaswa kutubeba kwa kuwa zinapotoa ushuru huondoka bila kutuchukua japo zipo baadhi zinazobeba abiria,” amesema mmoja ya abiria.
Abiria aliyejitambulisha kwa jina la Robson John amesema kilichopo hapo kwa sasa ni tabia ya baadhi ya daladala kuingia nje ya kituo hicho na kulipia uchuru kisha kuondoka bila kubeba abiria jambo ambalo limedumu kwa muda mrefu sasa bila kupatiwa ufumbuzi..
Amesema kilichotokea jana asubuhi ni kwam ba abiria walitoa malalamiko yao kwa ofisi inayotoza ushuru wa daladala hizo kwa kuitaja daladala yenye namba ya usajili. T 703 DKY Inayofanya safari zake Bunju Sokoni na Makumbusho kuwa ni kawaida yake kukataa abiria katika kitua cha Bunju Sokoni kila asubuhi kwa kisingizio kuwa ni bovu.
Mbali na changamoto hiyo ya asubuhi, inapofika jioni abiria hao hao hupata shida ya kulipa nauli mara mbili kwani daladala huishia kituo cha Bunju B badala ya kuishia Bunju Sokoni.
“Tatizo hili la kukatiza njia limekuwa sugu kwa barabara hii ya Bagamoyo,” amesema abiria mwingine.
Mvua za masika zilizonyesha kwa wingi mwaka huu, zilisababisha madereva wa daladala kukimbia kituo hicho na kila mmoja kushusha au kupakiza abiria sehemu yoyote wanaojisikia wao hali inayochangia usumbufu mkubwa kwa abiria.
Kwa upande wa Magari yanayoelekea Bagamoyo yametoka nje ya kituo na kushusha na kupakiza abiria karibu na barabara ya Bagamoyo.
Magari hayo ya Bagamoyo yanakutana na changamoto ya kuwakosa abiria kutokana na mkanganyiko huo uliopo, katika hili serikali inapaswa kuchukua hatua stahiki.
Mwandishi wa habari hii aliwasiliana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika halmashauri hiyo, Aquilinus Shiduki ambaye amesema Manispaa ya Kinondoni ipo kwenye mpango wa kuboresha hicho kituo, kwani wanazifahamu changamoto zinazowakumba abiria.