Na Lucy Lyatuu, Dodoma
MAENEO 65 katika Mikoa 14 nchini yametengwa na Tume ya Madini kwa ajili ya wachimbaji wadogo wenye umri unaoanzia miaka 18 hadi 40lengo likiwa ni kuhamasisha ushiriki wa vijana katika rasilimali za madini.
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume hiyo, Khamisi Kamando amesema hayo wakati , akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, akielezea mikakati ya tume hiyo pamoja na fursa zilizopo kwa vijana kwenye sekta ya madini.
Aidha amesema , katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, Serikali ilitoa leseni 5,983 za uchimbaji mdogo wa madini, ambapo asilimia 71 ya leseni hizo zilitolewa kwa vijana.
Kuhusu mikakati ya Tume na fursa kwa vijana nchini , amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuongeza ushiriki wa vijana katika sekta ya madini kupitia utoaji wa leseni, mafunzo, upatikanaji wa mitaji pamoja na kutenga maeneo maalum ya uchimbaji kwa wachimbaji wadogo.
Amesema Kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (MBT), leseni 273 zilitolewa kwa vikundi 183 vya vijana vilivyosajiliwa katika halmashauri mbalimbali, hatua iliyowezesha vijana 2,550 kupata ajira za moja kwa moja katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.
“Sekta hii imeendelea kukuza ujuzi wa vijana, ambapo wachimbaji wadogo zaidi ya mia Tano walipatiwa mafunzo ya uchimbaji, uchenjuaji, uongezaji thamani na biashara ya madini kupitia ushirikiano wa Tume ya Madini na Shirika la Madini la Taifa (Stamico),” amesema Kamando.
Kuhusu kuongeza thamani kwa madini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi, amesema hadi sasa kuna viwanda saba vya kusafisha madini vinavyofanya kazi nchini na kutoa ajira 273.
Kadhalika amesema Tume imejipanga kuongeza kiwango cha utafiti wa madini nchini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

