Na Lucy Ngowi
DODOMA; WAFUGAJI wengi nchini hawana ufahamu wa kutosha kuhusu Sheria ya Ustawi wa Wanyama, Sura Na. 154, hali inayosababisha baadhi yao kuwanyima huduma muhimu wanyama wao bila kujua kuwa ni kosa kisheria.
Wakili wa Serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT),
Vick Mbunde amesema hayo katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema lengo kuu la elimu hiyo ni kuwawezesha wafugaji kufahamu haki na ustawi wa wanyama wanaowafuga, pamoja na wajibu wao kisheria.
“Wafugaji wengi hawafahamu kuwa kuna sheria inayowataka l kuwahudumia vyema wanyama wao, ikiwa ni pamoja na kuwapatia chakula cha kutosha, maji safi, malazi bora na matibabu.
“Sheria hii inalinda wanyama dhidi ya mateso, manyanyaso na mazingira duni ya maisha,” amesema.
Amesema Sheria ya Ustawi wa Wanyama inatoa adhabu kwa mtu yeyote atakayekiuka masharti hayo, ikiwa ni hatua ya kulinda maslahi ya wanyama wanaofugwa na binadamu.
Katika maonesho hayo, Tume hiyo pia imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye maelezo ya msingi kuhusu sheria husika, sambamba na kutoa nafasi kwa wananchi kuuliza maswali na kupatiwa majibu ya kitaalamu kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu mifugo na wanyama kwa ujumla.
Hosea Godwin, mmoja wa wafugaji waliotembelea banda la Tume hiyo, amepongeza jitihada hizo na kusema kuwa elimu waliyopata imewasaidia kufahamu masuala ambayo hapo awali walikuwa hawajayazingatia.
“Nilikuwa sifahamu kuwa ukimtesa mnyama, kama kumpiga au kumwacha bila chakula kwa siku kadhaa, ni kosa linaloweza kupelekea kuchukuliwa hatua za kisheria. Hii ni elimu muhimu sana kwetu wafugaji,” amesema Hosea.