Na Shani Kibwasali
MBEYA: KIKAO cha Kwanza cha Kamati Kuu ya Maandalizi ya Sherehe ya Mei Mosi Kitaifa, 2025 kimekutana mkoani Mbeya ambako maadhimisho hayo yatafanyika.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera alilishukuru Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), kwa kuteua mkoa huo kuwa mwenyeji wa Sherehe za Wafanyakazi kitaifa kwa mwaka huu 2025.
Homera amesema uchaguzi huo ni heshima kubwa kwa kuwa sherehe hizo zingeweza kufanyika katika mkoa mwingine wowote.
Amewakaribisha wafanyakazi wote na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kujisikia wako nyumbani, ikiwa ni pamoja na kuwaomba washirikiane na wenyeji ili wafanikishe sherehe hizo.
“Maadhimisho yatafanyika pasipo na shaka kwa kuwa kila mmoja ni mfanyakazi katika eneo lake. Ni muhimu na jambo jema kuichukulia kwa upekee, siku hii ya wafanyakazi Mei Mosi,” amesema.
Naye Rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya ameushukuru uongozi wa mkoa kwa kuridhia sherehe hizo kufanyika Jijini Mbeya.
Pia amewakumbusha wajumbe wa kamati za maandalizi kuwa Mei Mosi ni kumbukumbu ya yale yaliyowahi kufanyika na wafanyakazi enzi za ukoloni wakati wakipigania haki za mfanyakazi ulimwenguni kipindi cha Mapinduzi ya Viwanda.
“Mei mosi si Vita kati ya waganyakazi na serikali, isipokuwa ni siku ambayo wafanyakazi hupenda kuwasilisha katika serikali yao yale ambayo wangependa serikali iyafanye ili kuboresha maslahi na ustawi wa mfanyakazi mahali pa kazi,” amesema.
Nyamhokya amemhaidi mkuu huyo wa mkoa ushirikiano kutoka katika vyama vya wafanyakazi vilivyo chini ya TUCTA, katika mchakato mzima wa kufanikisha maadhimisho hayo.
Pia amewataka wajumbe wa kamati mbalimbali katika kikao hicho, kuipokea sherehe hiyo Mkoani mbeya, ikiwa ni pamoja na kushiriki ipasavyo kuifanikisha, kwa kuwa jiji hilo la Mbeya limepewa nafasi ya pekee kwa mwaka huu 2025.
Amewataka wajumbe walioteuliwa katika kamati mbalimbali kufanya kazi kwa kujituma ili kufanikisha sherehe hiyo kwa kuwa wao ndio taswira nzima ya mafanikio ya sherehe.
Amesema uwepo wa sherehe hiyo mkoani Mbeya ni fursa kwa wakazi wa mkoa huo, wakiwemo wafanyabiashara kwa kuwa kwa nyakati tofauti kutakuwa na watu wengi wakitumia na kununua bidhaa mbalimbali hadi kilele cha maadhimisho.
Awali Naibu Katibu Mkuu TUCTA, Rehema Ludanga alielezea malengo ya kikao hicho.
Ludanga amesema lengo la kijao hicho ni kupanga namna bora ya kufanikisha sherehe hizo.
Kikao hicho kimewashirikisha viongozi wakuu wa vyama vya wafanyakazi nchini, viongozi wa serikali ya Mkoa wa Mbeya, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama y Mkoa