
Aidha ameielekea TTCL kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa gharama nafuu kwa kuandaa vifurushi vinavyokidhi uwezo wa familia, wanafunzi, vijana na wafanyabiashara wadogo na wa kati.

Amesisitiza uwajibikaji na nidhamu ya kibiashara katika usimamizi wa mradi, akitaka wazabuni na wakandarasi wasimamiwe kwa ufanisi ili kazi zikamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia thamani ya fedha inayowekezwa.
Amesema mradi huo unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali 2024–2034, unaolenga kuongeza matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa huduma za Serikali kwa njia ya kidijitali.
Waziri Kairuki, amesema katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inakusudia kuhakikisha ifikapo mwaka 2050 angalau asilimia 70 ya wananchi wanatumia TEHAMA, huku zaidi ya asilimia 80 ya huduma za Serikali zikipatikana kwa njia ya kidijitali iliyo salama na jumuishi.

Akitumia takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo mwaka iliyoishia Juni 2026, Waziri Kairuki amesema usajili wa intaneti nchini umefikia 62,793,986, huku matumizi ya data yakifikia Petabaiti 1,041.
Hata hivyo, amesema usajili wa huduma ya Faiba Nyumbani ulikuwa 178,904, hali inayoonyesha kuwa bado kuna fursa kubwa ya kukuza huduma ya intaneti ya kasi kupitia teknolojia ya nyuzi za macho.
Amesema TTCL imeingia katika Awamu ya Pili ikiwa tayari imejenga msingi muhimu kupitia utekelezaji wa Awamu ya Kwanza, iliyolenga maeneo mbalimbali ya kimkakati nchini.
Amesema katika Awamu ya Kwanza, TTCL imefanikiwa kujenga zaidi ya Home Pass 280,000, huku jumla ya maungio ya huduma ya nyuzi za macho yakifikia karibu 300,000 nchini.

Aidha amesema utekelezaji wa mradi huo unafanyika kwa ushirikiano na makandarasi wa ndani na wa kimataifa, wakiwemo Huawei, ZTT na Visoll, katika ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya nyuzi za macho.

Amesema ushirikiano huo ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha upanuzi wa mtandao unafanyika kwa kutumia teknolojia za kisasa na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za intaneti nchini.
Mradi huo unalenga pia kuchochea matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku, biashara, elimu na huduma za Serikali, sambamba na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia upatikanaji wa intaneti yenye kasi na uhakika.


