Na Lucy Lyatuu
SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limesema litaendelea kuboresha mifumo yao kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza thamani katika huduma wanazotoa kila siku.
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL Humphrey Ngowi amesema hay oleo Dar es salaam wakati akizungumza katika hafla ya kufunga Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka 2025.
Amesema kwa miaka mingi TTCL imeendelea kuwa nguzo ya mawasiliano nchini kwa kutoa huduma muhimu zinazowaunganisha Watanzania mijini na vijijini.
“Shirika linatambua kuwa dunia ya sasa inabadilika kwa kasi, na tunaona ipo haja ya kuendelea kuboresha huduma zetu kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, za kuaminika na zenye ubora wa hali ya juu,” amesema Ngowi.
Amefafanua kuwa, kwa mwaka huu TTCL imefanya maboresho makubwa kupitia miradi ya kimkakati ikiwemo kupanua huduma vijijini na mijini, kuendeleza upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, pamoja na kusimamia ujenzi wa minara mipya ya mawasiliano nchini.

Kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Ngowi amesema wiki hiyo imeacha alama ya kudumu ndani ya shirika hilo kwa kuwa imekuwa fursa ya kukusanya mrejesho kutoka kwa wateja, kutambua mapungufu na kuandaa maboresho yanayolenga kukidhi mahitaji ya wananchi.
“Mafanikio tuliyoyapata tusingeweza kuyafikia bila ushirikiano wa wateja wetu. Ndio sababu kuu ya sisi kuwepo, na kupitia kwao tunathibitisha kuwa Mission Possible sio kaulimbiu tu, bali ni uhalisia tunaouishi kila siku,” amesisitiza Ngowi.
Ameahidi kuwa TTCL itaendelea kusikiliza maoni ya wateja na kuyafanyia kazi ili kuhakikisha kila mmoja anapata thamani stahiki ya huduma anayostahili.
Hata hivyo katika kufunga wiki hiyo amewashukuru wateja wao kwa michango na juhudi zao katika Nyanja mbalimbali.

“Tukiwa na kaulimbiu ya Mission Possible, naamini tutafanikisha mambo makubwa zaidi katika siku zijazo,” amesema Ngowi.