Na Mwandishi Wetu
BURUNDI: Kutokana na kutiwa Saini utekelezaji wa Mradi wa SGR awamu ya pili, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limefanya ziara nchini Burundi kwa ajili ya kukutana na wadau mbalimbali.
Utiwaji Saini huo awamu ya pili ya kipande cha saba kutoka Uvinza Tanzania na kipande cha nane kutoka Malagarasi – Msongati, Burundi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu nchini Burundi, Nijimbere Egide ameeleza ziara hiyo imefanywa katika mikoa ambayo mradi wa SGR unatarajiwa kupita ikiwemo Mkoa wa Makamba na Rutana, ameihakikishia TRC kwamba wananchi wako tayari kutoa maeneo yatakayohitajika ili kurahisisha ujenzi.
“Nawahakikishia kwamba sheria ya Burundi, iko vizuri katika utwaaji ardhi ya wananchi na wao wako tayari kwa asilimia 100,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Wataalamu wa Mradi wa SGR kipande cha saba na nane, Benjamin Mbimbi amesema wananchi nchini Burundi watanufaika katika mambo mbalimbali ikiwemo miji kukua kibiashara kutokana na wageni watakao ingia na kutoka, kujengwa kwa shule, hospitali katika maeneo yaliyopitiwa na mradi pamoja na fursa mbalimbali za ajira katika maeneo hayo.
“Mradi unapokuja katika nchi, ni jukumu la wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji ikiwemo sekta ya hoteli na huduma nyingine za kijamii,” amesema.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa miundombinu kutoka TRC Machibya Masanja amesema mantiki ya mradi huo ni kuunganisha mgodi wa Msongati na Bandari ya Dar es Salaam, pia kuweka mtangamano wa kibiashara kati ya nchi ya Burundi na Tanzania.
“Tanzania tunawapa huduma wenzetu ambao hawana bahari waweze kutoa bidhaa kutoka kwenye masoko yao kama mgodi wa msongati kuelekea masoko ya nchi za Ulaya na nchi nyingine,” amesema.
Amesema gharama za uwekezaji wa mradi huo unagharimu dola za kimarekani bilioni 2.154 ambapo utekelezaji wa mradi huo utachukua miezi 72, miezi 60 ya ujenzi wa reli ikijumuisha miezi 12 ya uangalizi.
“Kipande ni kifupi lakini kutokana na sababu za kijografia nchi ya Burundi kuwa na milima mingi hivyo inahitaji mahandaki na madaraja makubwa,” amesema.
Mkataba wa Mradi huo ulisainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, Januari 29 mwaka huu 2025, Stesheni ya Magufuli Jijini Dae es Salaam,