Na Lucy Ngowi
DODOMA: MKURUGENZI Mkuu wa, Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA),Profesa Joseph Ndunguru amesema Wamefanikiwa kudhibiti ugonjwa usiojulikana uliosababisha kunyauka kwa mimea ya viazi mviringo.
Ugonjwa ambao ulioathiri wakulima wa Tarafa za Ikuna, Kichiwa na Mtwango mkoani Njombe.
Profesa Ndunguru alieleza hayo, alipokuwa akitoa taarifa ya mamlaka hiyo kwa vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya mwaka 2023/2024 hadi 2025/2026,

Alisema ugonjwa huo ulisababisha hasara kubwa kwa wakulima waliokuwa wamenuia mbegu za viazi aina ya Sagitta na Cayman, waliopata mkopo kutoka Benki ya CRDB.
“Uotaji na ukuaji wa mbegu ya Cayman ulikuwa mbaya, na hasara ilifikia takriban Sh. Bilioni 1.3, huku wakulima wakishindwa kurejesha mikopo yao,” alisema Profesa Ndunguru.
Alisema TPHPA ilichukua sampuli za mimea iliyoathirika na kutumia kipimo cha PCR kubaini chanzo cha ugonjwa.

Alieleza, uchunguzi ulionyesha kuwa bakteria Pectobacterium spp na Dickeya spp ndio walikuwa chanzo cha ugonjwa huo, na mamlaka hiyo ilipendekeza njia za udhibiti ili kuzuia kuenea zaidi.
Profesa Ndunguru aliongeza kuwa ripoti ya uchunguzi iliwezesha wakulima kushirikiana na benki ya CRDB, jambo lililowafanya kuongezewa muda wa kulipa mikopo katika msimu uliofuata wa kilimo.
Aidha, TPHPA pia imefanikiwa kudhibiti Funza Weupe katika Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, hasa katika kata ya Kilimampimbi na vitongoji vya Ikomela, Mavula, Waya na Rupia, vilivyoashiria hatari kwa mazao ya wakulima.

Alisisitiza kuwa, hatua hizo zimeongeza ulinzi wa mazao, kupunguza hasara kwa wakulima, na kuhakikisha mazao bora yanapatikana kwa msimu ujao wa kilimo.

