Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), imekuwa ikielekeza wakulima namna ya kutumia viuatilifu kwa usahihi kwa kuwa wakati mwingine huchanganya viuatilifu vya magonjwa na vya wadudu hivyo kupunguza ufanisi.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru ameeleza hayo kwenye kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na maonesho linalomalizika leo jijini Dar es Salaam.
“Kwa mfano katika msimu wa kilimo uliopita tuliamua ugawaji wa kiuatilifu cha sulphur kwa wakulima wa korosho mikoa ya Lindi na Mtwara lazima uendane na mafunzo.

” Kwa hiyo wakati viuatilifu vinagawiwa timu kutoka TPHPA ilikuwa sambamba ikielekeza namna ya kutumia viuatilifu, imeleta tija hiyo ni endelevu tunaendelea kwa mazao mengine,” amesema.
Pia ameeleza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikichukua sampling ya mazao kwenye masoko ya ndani lakini pia kwenye mashamba ya wakulima kabla hayajaenda sokoni ili kuhakikisha kwamba mazao yale hayana masalia ya viuatilifu.
Amesema wanafanya hivyo kupunguza athari kwa binadamu lakini pia wanafanya na mafunzo ambayo mpaka sasa wamemaliza Zanzibar, Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam na Iringa, wanaendelea na mikoa mingine.
Awali amesema mamlaka hiyo moja ya kazi yao ni kusimamia matumizi salama ya viuatilifu ili kulinda afya za walaji, wanyama na mazingira.
Amesema wanatoa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya viuatilifu kwa wauzaji wa bidhaa hiyo kwa kuwa ipo kisheria.
“Mtu kabla hajaingia kwenye biashara ya kuuza viuatilifu lazima apate mafunzo,” amesema.