Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: TOLEO la Sheria ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili zitaanza kutoka Agosti mwaka huu 2025.
Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, amesema hayo katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Njole amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye aliagiza sheria za nchi kutafsiriwa ili kuwawezesha wananchi wa makundi yote kuzielewa kwa urahisi.
“Pamoja na hatua kubwa ya urekebu wa sheria iliyofanyika, Rais aliagiza pia kukamilishwa kwa zoezi la kutafsiri sheria kwa Kiswahili. Hii ni kwa sababu wananchi wengi hawana uelewa wa lugha ya kisheria ya Kiingereza,” amesema.
Kwa mujibu wa Njole, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanya kazi kubwa ya kurekebisha sheria zilizopo ili ziendane na mazingira ya sasa ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia, ikiwa ni pamoja na kuanza mikakati ya kutunga sheria mpya zitakazodhibiti matumizi ya teknolojia ya Akili Bandia.
“Tunaandaa mfumo maalum wa kisheria wa kusimamia matumizi ya Akili Mnemba (AI), na utakapokamilika, Miswada ya sheria itapelekwa bungeni kwa ajili ya kuundwa sheria kamili,” amesema.
Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu Msaidizi wa Sheria, Rahema Katuga amesema marekebisho ya sheria yaliyokamilika hivi karibuni yameanza kutumika rasmi tangu Julai mosi mwaka huu, 2025, na sheria za zamani ambazo hazijafanyiwa urekebu hazitatumika tena.
“Kuanzia sasa, mtu yeyote anayetaja kifungu cha sheria katika mazingira ya kimahakama au kiofisi, anatakiwa kutumia marejeo ya sheria mpya zilizorekebishwa,” amesema.
Hatua hii inaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za serikali za kukuza ushirikishwaji wa wananchi katika masuala ya kisheria, kuimarisha utawala wa sheria na kukuza matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kisheria na ya taifa.