Na Mwandishi wetu, Nzega Tabora
SEKTA ya Kilimo inatajwa kuwa mhimili wa uchumi wa Tanzania, ikiajiri takribani theluthi mbili ya nguvu kazi ya taifa na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda, asilimia 100 ya usalama wa chakula, na zaidi ya asilimia 26 ya pato la taifa.
Akizungumza katika mkutano na wakulima katika kijiji cha Ndala Wilayani Nzega Mkoa wa Tabora, Mkuu wa Wilaya hiyo Naitapwaki Tukai amesema, maendeleo ya mwananchi na taifa yanategemea ufanisi katika sekta ya kilimo hivyo ni wajibu wa kila mkulima kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea.
Amesema bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi trilioni 1.24 mwaka wa fedha wa 2024/25 ambapo lengo hasa ni kufanya mapinduzi katika Sekta ya Kilimo kwa kuongeza tija.
Aidha aliongeza kuwa Serikali imeendelea kutoa mbolea kwa bei ya ruzuku kwa misimu mitatu mfululizo, kuhakikisha mkulima anapata mbolea kwa bei himilivu na kuwakumbusha wakulima kuitumia mbolea hiyo kwa usahihi ili ilete matokeo mazuri wakati wa mavuno.
“Tukipata matokeo mazuri wakati wa mavuno tutakua na uhakika wa chakula kwa mkulima mmoja mmoja, uhakika wa chakula kwa Taifa letu lakini pia tutapata ziada kwaajili ya biashara ili kukidhi mahitaji mengine ya familia”, aliongeza.
Naye mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Anthony Diallo alitumia wasaa huo kuwakumbusha wakulima kutumia mbolea sahihi, kwa wakati sahihi, kwa kipimo sahihi na eneo sahihi la mmea.
“Ndugu zangu wakulima leo tumekusanyika hapa ili tukumbushane kupitia kampeni yetu ya Kilimo Ni Mbolea tuone mabadiliko katika mavuno yetu kwa kuzingatia kanuni nne muhimu za matumizi sahihi ya mbolea ili tuendelee kupata mavuno mengi na bora”,alisema Dkt. Diallo.
Pamoja na hilo Dkt. Diallo aliwakumbusha wakulima kusajiliwa kwenye daftari la wakulima na kuingia kwenye mfumo wa kidigitali wa mbolea ya ruzuku ikiwa ni moja kati ya hatua muhimu kwa uzalishaji tija na ukuaji wa sekta ya Kilimo nchini.
“Kwasababu Kilimo ni Mbolea hatuna budi kuchangamkia fursa ya usajili tukiwa na kitambulisho cha NIDA au cha mpiga kura baada ya hapo tutumie mbolea kwa kuzingatia kanuni nne muhimu za mbolea ambazo ni nunua mbolea sahihi, tumia mbolea kwa wakati sahihi, kwa kipimo sahihi na sehemu sahihi, kwa kuzingatia hayo tutaendelea kuneemeka kwa chakula na kipato pia”, alibainisha Dkt. Diallo.
Vilevile Dkt. Diallo aliongeza kuwa kwa kusajiliwa na kuoata mbolea ya ruzuku wakulima watakua wameifanikisha azma ya Serikali, ya kukifanya Kilimo kiwe biashara na sio adhabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Joel Laurent alisema kuwa TFRA inafanya kampeni ya Kilimo ni mbolea katika maeneo tofauti nchini ili kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha wakulima kujisajili kwenye daftari la wakulima ili wanufaike na mbolea za ruzuku.