Dar es Salaam: WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wameendelea kuunga mkono jitihada za serikali za matumizi bora ya nishati safi, kwa kutoa elimu ya ufugaji nyuki ambayo itamwezesha mwananchi kupata kipato kizuri bila uchafuzi wa mazingira.
Aidha katika jitihada hizo za kudhibiti uharibifu wa misitu, wakala huo imepandisha hadhi baadhi ya misitu na kuwa Hifadhi za Mazingira Asilia, ambako kunafanyika shughuli za utafiti na utalii ambao unawezesha TFS kupata fedha.
Mhifadhi Mkuu TFS Kassim Ally amesema hayo alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Televisheni moja hapa nchini.
Amesema mtu anapofuga nyuki faida yake inapatikana kwenye asali ambayo inamwezesha kupata kati ya sh 10,000 na 15,000 kwa kilo moja.
Ally amesema mwananchi anapoharibu msitu mkoa mojawapo anaathiri nchi nzima sio mkoa huo pekee, hivyo TFS inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha elimu ya uharibifu wa mazingira na utumiaji wa nishati safi inawafikia watanzania.
Amesema japokuwa mkoa wa Dar es Salaam una nishati ya gesi na umeme, unaoongoza kwa utumiaji wa kuni.
“Dar es Salaam ndio unatumika sana mkaa, magunia zaidi ya 500,000 yanaingia kila mwezi, amesema na kuongeza kuwa watu wamekuwa wakitumia kuni na mkaa kimazoea tu,” amesema.
Amesema kwa kijijini mkaa na kuni ndio unaowaingizia kipato hivyo wanaendelea kutoa elimu iweze kuwafikia.
Amesema watu wanaangusha miti tani 10 hadi 12 wanapotengeneza mkaa huata tani moja pekee.