Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: TEKNOLOJIA mpya inayotumia mashine ya kuchochea mafunzo ya uchomeleaji imeleta mapinduzi makubwa katika mbinu za kufundishia uchomeleaji kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi nchini.
Mkufunzi kutoka Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma (VETA) Dodoma,
Manfred Mapunda amesema hayo katika maonesho ya 49 ya Kumataifa ya Biashara yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema awali walikuwa wakifundisha wanafunzi kwa kutumia vifaa halisi moja kwa moja, jambo lililosababisha upotevu mkubwa wa malighafi kutokana na makosa ya mara kwa mara ya wanafunzi wakati wa mazoezi ya uchomeleaji.
“Mwanafunzi alipokosea, alilazimika kutumia vifaa vingine tena na tena, na hivyo kufanya chuo kupoteza vyuma vingi na kugharimu fedha nyingi,” amesema.
Amesema teknolojia hiyo mpya imesaidia kupunguza gharama na upotevu wa vifaa kwa kiasi kikubwa.
“Mashine hii huwapa wanafunzi nafasi ya kujifunza kwa njia ya majaribio ya kielektroniki, ambapo wanaweza kurudia mazoezi mara nyingi bila kutumia vyuma halisi.
“Mwanafunzi anaweza kurudia zoezi zaidi ya mara 10 hadi afanikiwe, bila kuchoma au kukata vyuma halisi,” amesema.
Ameongeza kuwa mbali na kupunguza gharama, teknolojia hiyo imesaidia kuongeza ufanisi katika ufundishaji.
Amesema awali idadi ya wanafunzi darasani ilipaswa isiwe zaidi ya 25 ili mwalimu aweze kuwafundisha kwa ufanisi. Lakini kupitia mfumo wa kuonyesha picha kwa kutumia projjekta sasa mwalimu anaweza kufundisha hadi wanafunzi 50 kwa wakati mmoja, huku kila mmoja akiwa na uwezo wa kuona kinachofanyika moja kwa moja ukutani.
Amesema teknolojia hiyo pia imeongeza hamasa miongoni mwa vijana, hususan wanafunzi wa kike, kushiriki katika fani ya uchomeleaji.
“Inawapa wanafunzi ujasiri na kujiamini katika kazi hii, ambayo si tu inatoa ajira bali pia kipato na fursa ya kuajiri wengine,” amesema.
Serikali kupitia VETA imeamua kuwekeza katika mashine hizo ili kusaidia katika uboreshaji wa elimu ya ufundi, kuongeza tija na kuandaa vijana kwa soko la ajira la sasa na la baadaye.