Na Mwandishi Wetu
Unguja: MaAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imeanza rasmi utekelezaji wa miradi ya amali kwa upande wa Zanzibar, ambapo Sh. Bilioni 3.2 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za mafunzo ya amali.
Katika kikao kazi kilichofanyika Aprili 8, 2025 kwenye ukumbi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali (WEMA) kisiwani Unguja, Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dkt. Erasmus Kipesha amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa mamlaka,

Kuhakikisha mafanikio ya uboreshaji wa Sera ya Elimu na mtaala mpya unaolenga elimu jumuishi na ya vitendo.
Dkt. Kipesha ameeleza kuwa miradi hiyo itajumuisha ujenzi wa madarasa na karakana zitakazotumika kwa ajili ya mafunzo ya vitendo, ambapo wanafunzi watapata ujuzi wa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi baada ya kuhitimu masomo yao.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu – Utawala Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khalid Waziri, ameshukuru na kuipongeza TEA kwa utekelezaji wa miradi hiyo kwani asilimia kubwa ya shule zilizopo visiwani Zanzibar hazina miundombinu ya amali.

Amesema miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa kwa jamii, kwani itawezesha vijana kupata ujuzi wa vitendo utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Waziri amefafanua kuwa Wizara ya Elimu imetenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo, moja ikiwa Unguja na nyingine Pemba ili kuhakikisha kuwa watoto wa Zanzibar wanapata fursa sawa ya elimu.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utasimamiwa kikamilifu na Wizara ili kuhakikisha kuwa unakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa na kwamba shule hizo zitakuwa na madarasa kwa ajili ya masomo ya nadharia na karakana kwa ajili ya mafunzo ya vitendo.

Kazi ya ujenzi wa shule hizo inatarajiwa kuanza mara moja, huku hatua za awali za usanifu wa michoro, upatikanaji wa vifaa vya ujenzi na maandalizi ya maeneo zikiendelea.
Miradi hiyo itahusisha ujenzi wa shule mbili, ambapo kila shule itakuwa na wastani wa amali tatu zinazotolewa kwa wanafunzi.
Ujenzi wa shule hizo unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu visiwani Zanzibar kwani itatoa fursa kwa vijana wengi kujiendeleza katika fani mbalimbali za amali.
Miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuhakikisha kuwa Watoto wote wanapata elimu bora na yenye tija inayozingatia mahitaji ya soko la ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
Huo ni muendelezo wa jitihada za Serikali za kuboresha sekta ya elimu, ni sehemu ya mkakati wa kuunga mkono Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Muda Mrefu wa Taifa 2011/12 hadi 2024/25.
Miradi hyo inalenga kutoa elimu ya vitendo inayokidhi mahitaji ya soko la ajira na kukuza ujuzi wa vijana ili kuchangia kwa ufanisi katika maendeleo ya Taifa.