Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imetenga Sh. Milioni 300 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la Bodi ya Maktaba lililopo Kisiwani Pemba.
Ukarabati unaolenga kuimarisha miundombinu ya taasisi hiyo muhimu inayotoa huduma kwa wanafunzi na wananchi kwa ujumla.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi kutoka TEA, Masozi Nyirenda amesema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi Kisiwani Pemba.
Nyirenda amesem fedha hizo tayari zimetolewa, na ukarabati utaanza mara tu baada ya mkandarasi kusaini mkataba rasmi na kuwasilisha mpango kazi utakaoonesha hatua kwa hatua namna kazi hiyo itakavyotekelezwa hadi kukamilika kwa wakati.

Naye Mratibu wa Bodi ya Maktaba Pemba, Ahmed Hamis amesema jengo linalotarajiwa kukarabatiwa ni miongoni mwa majengo ya kihistoria yaliyojengwa kipindi cha ukoloni.
“Hata hivyo, tangu lijengwe, jengo hilo halijawahi kukarabatiwa, jambo lililosababisha uchakavu mkubwa wa jengo zima na miundombinu ya ndani, na hivyo kuathiri utoaji wa huduma kwa wananchi,” amesema.
Amesema kukamilika kwa ukarabati huo kutakuwa ni faraja kwa wakazi wa Wilaya jirani ambao hutegemea huduma za maktaba hiyo kwa ajili ya kusoma vitabu, hasa watoto wanaohitaji nyenzo za kielimu kama vile hadithi na historia za watu mashuhuri.

Mradi huo wa ukarabati unatekelezwa kama sehemu ya majukumu ya TEA kama taasisi ya Muungano, ambayo kimsingi inahusika na utafutaji wa rasilimali kutoka kwa wadau mbalimbali ili kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Kupitia miradi kama hiyo, TEA inalenga kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata mazingira bora ya kujifunzia bila kujali eneo analotoka.