Na Lucy Ngowi
CHAMA cha Mabaharia Tanzania (TASU), kinaiomba serikali inunue au kutengeneza meli hata moja kwa ajili ya mizigo nje ya nchi na kuileta Tanzania ili vijana wanaomaliza vyuo wapate ajira.
Kaimu Katibu Mkuu wa TASU, Hamis Urembo amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Mfanyakazi.
Urembo ameomba ombi hilo kwa kuwa hivi sasa ajira za mabaharia zimekuwa chache, ilhal chuo cha bahari kikiwa kinazalisha wanafunzi wengi kila mwaka ambao wanazagaa mitaani kwa kuwa hakuna meli za kuwasaidia.
“Sasa hivi tuna kiwanda kinatengeneza meli. Itengenezwe meli au inunuliwe nje ya nchi.
“Hapo zamani tulikuwa na kampuni ya ushirikiano ya meli ya China na Tanzania. Tulikuwa na meli nyingi kama MV Ruaha, MV Urafiki,
“Kupitia chama cha mabaharia kila baada y miezi sita tulikuwa tunachukua mabaharia kwetu sisi, wanakwenda China, wanafanya kazi miezi sita, baada ya miezi sita wanapokezana, sisi tunafanya kazi kwa mkataba,” amesema.
Amesema bahati mbaya zile meli zimeuzwa, na hiyo kampuni ya China imeuza meli zote, japo bado ipo.
Amesema kama serikali ingeweza kukaa nao na kuanza upya ushirikiano uliokuwepo ili wanunue meli.
Kwa upande mwingine amesema, changamoto nyingine iliyopo katika fani hiyo hakuna mwongozo wa ajira kwa kutoa mfano kwamba Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), inaweza kutangaza nafasi za kazi.
Kwamba wanahitaji mabaharia na wanatambua vyeti , inapofikia kwenye maslahi na malipo hawatambuliwi vyeti.
” Kwa mfano mtu anasoma chuo cha baharia anapata vyeti vyake na kuwa nahodha lakini akipata kazi haitwi nahodha anaitwa dereva wa vivuko.
“Hiyo ni changamoto ambayo inatufanya sisi tuwe na matatizo hayo,” amesema.
Pia amesema ni muhimu kuwe na sera ya bahari kuondoa changamoto mbalimbali.