Na Lucy Ngowi
GEITA: SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepiga marufuku kwa kampuni binafsi kushiriki katika shughuli za usafirishaji na uondoaji wa kemikali hatarishi na vilipuzi vinavyotumika kwenye migodi, likisisitiza kuwa kazi hiyo ni ya shirika hilo pekee kwa mujibu wa sheria.
Mkurugenzi wa Huduma za TASAC, Hamid Mbegu amesema hayo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyomalizika jana Septemba 28, 2025 mkoani Geita.

Amesema kumekuwepo na ukiukwaji wa sheria ambapo baadhi ya makampuni binafsi yamekuwa yakihusika na usafirishaji wa shehena hizo hatarishi, kinyume cha taratibu.
“Baadhi ya shehena hizi ni sumu na zina madhara makubwa. Serikali kupitia TASAC ndiyo yenye mamlaka ya kisheria kusimamia na kuratibu uondoshaji wa kemikali hizo. Tunasisitiza kuwa hakuna kampuni binafsi inayopaswa kujihusisha na kazi hii,” amesema Mbegu.
Ameongeza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli, Sura 415, Kifungu Na.7, TASAC ndiyo taasisi pekee ya serikali yenye jukumu la kusimamia masuala yote ya ugomboaji na uondoaji wa shehena hatarishi, ikiwemo kemikali kama Sodium Cyanide, inayotumika katika shughuli za ulipuaji na usafishaji wa madini.
TASAC imetoa rai kwa wachimbaji wakubwa na wadogo, pamoja na kampuni za uagizaji na uondoaji wa mizigo, kuhakikisha wanazingatia sheria na kuepuka kutumia kampuni zisizoidhinishwa, kwani kufanya hivyo ni kukwenda kinyume cha sheria za nchi.
Maonesho ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora katika sekta ya madini, huku yakihusisha wadau mbalimbali wakiwemo wachimbaji, taasisi za serikali, watafiti na wawekezaji.